Home » » TRA Mara yakusanya bil. 79/-

TRA Mara yakusanya bil. 79/-



WAFANYABIASHARA mkoani Mara, wametakiwa kulipa kodi kwa wakati kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa kuzingatia taratibu mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja kuwapatia risiti wateja pindi wanapowauzia bidhaa.
Wito huo ulitolewa jana na meneja wa TRA mkoani hapa, Joseph Kalinga, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mlipa kodi zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo mjini Musoma.
Aliwataka wafanyabiashara kujijengea mazoea ya kulipa kodi zao kwa wakati bila udanganyifu ikiwa ni pamoja na kuwasihi kutoa risiti kwa wateja wao kwa bidhaa wanazokuwa wameuza ili kufanikisha mpango wa ulipaji kodi.
Awali akisoma taarifa ya makusanyo ya mkoa, Kalinga alisema TRA mkoani hapa imekusanya zaidi ya sh bilioni 79 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kiasi ambacho ni zaidi ya lengo lililokusudiwa la zaidi ya sh bilioni 68, sawa na asilimia 116.1.
Aidha Kalinga ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha ulioanzia Julai 2013/2014 TRA imekusanya zaidi ya sh bilioni 24, sawa na asilimia 91.24, huku wakitaraji kukusanya zaidi ya sh bilioni 110.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Mara, Bartazal Bibogo, amezitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya uchumi mkoani hapa kuwa ni pamoja na kufa kwa viwanda, uzalishaji wa chini ya kiwango pamoja na miondombinu mibovu.
Alisema kama viwanda na miundombinu ikiimarishwa, mamlaka hiyo itaweza kuchangia ukuaji uchumi kwa makusanyo makubwa ya kodi.
Gibogo amevitaja baadhi ya viwanda vilivyokufa na vingine kufanya chini ya kiwango kuwa ni pamoja na Mutex, Vilian, Musoma Fish Processors na Prime Ketchi; na kuongeza kuwa serikali na uongozi wa viwanda wanapaswa kukaa pamoja ili kuangalia chanzo cha kufa au kufanya chini ya kiwango kwa viwanda hivyo.

Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa