Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele
Tuhuma hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime, Amos Sagara katika kikao kilichoitishwa na Katibu wa Itikani na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye kwa kusikiliza kero ambazo zimekuwa zikisabisha mahusiano mabaya kati ya wananchi na uongozi wa mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold.
Katika kikao hicho kilichofanyika juzi katika mji mdogo wa Nyamongo na kuhudhuriwa na mkuu huyo wa wilaya, wakiwamo viongozi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo na wawakilishi wa wananchi, kiongozi huyo wa halmashauri ya Tarime alidai DC Henjewele amekuwa chanzo kikuu cha kukosekana kwa amani katika eneo hilo.
Alisema baada ya kuanzishwa mfuko wa elimu kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wa vyuo mbalimbali wanaotoka katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo, alidai kuwa mkuu huyo wa wilaya alizuia fedha hizo kuwekwa katika mfuko huo badala yake zinapelekwa ofisini kwake hatua ambayo imeshindwa kuwasaidia wananchi hao na hivyo kuzua mgogoro mkubwa.
“Tatizo la hapa ni DC (mkuu wa wilaya) amekuwa akitumia fedha za mfuko wa elimu kama NGOs yake kila kitu yeye amekuwa kinga kwa mgodi kushindwa kutekeleza mikataba…kila kitu ukiuliza unaambiwa muulize DC hivi huyu mkuu wa wilaya ni nani katika mgodi wa North Mara?” alihoji Sagara huku akishangiliwa na viongozi wa vijiji na wawakilishi wa wananchi.
“Kila tukidai haki za wananchi wetu ambazo zinaonekana kuporwa na mgodi, unakutana na vizingiti vingi eti unakuta DC anawajibia mgodi hauna fedha …hii ni hatari sana bila kuchukua hatua dhidi ya mkuu wa wilaya tatizo hili la mgogoro kamwe haliwezi kuisha” aliongeza.
Mkazi mmoja wa Nyamongo, Daud Makone alimtuhumu mkuu huyo wa wilaya kuchangia kuvuruga mahusiano mazuri yaliyokuwapo kati ya wananchi na uongozi wa mgodi huo.
“Miaka yote tumekuwa tukihamishwa bila vurugu wala watu kutishwa, tena tunapokea fidia na kuondoka …sasa tangu amekuja huyo mkuu wa wilaya imekuwa kero kubwa hatua ambayo imefanya kuwapo kwa uhasama mkubwa kati ya jamii na uongozi wa mgodi” alisema.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya ya Tarime, Henjewele, alikanusha kuhusika na ubadhirifu wa fedha hizo za mfuko wa elimu, huku akisema hajawahi kuchukua fedha hizo kusomesha mtoto wake.
“Naomba mthibitishe hapa kama kweli kuna jina la mtoto wangu ambaye amewahi kusomeshwa na fedha za mgodi, tulifanya uchunguzi tukabaini kuwa fedha hizo zimekuwa zikichakachuliwa na baadhi ya watumishi wa mgodi na tulipobaini tu tulichukua hatua ya kumwambia meneja wa mgodi na tayari watumishi wengine wamefukuzwa kazi” alisema na kuongeza.
“Pia kuna baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa vijiji wamekuwa wakiingiza majina hewa ambao si wahitaji wa kusomeshwa wa fedha hizo hatua ambayo ilisabisha mgodi kushindwa kuchangia fedha katika mfuko huu, sasa leo iweje mseme DC ndiye anahusika, mimi nafanya kazi kwa kufuata taratibu” alisema Henjewele.
Akizungumza katika kikao hicho, Nape Nnauye, alisema CCM haitakubali kuendelea kwa uhasama katika eneo hilo huku wananchi wakikosa haki zao kutokana na tamaa za baadhi ya viongozi.
“Nimesema nakwenda kukutana na Tamisemi ili watume watu wao kuja kuchunguza, tukibaini yoyote aliyehusika bila kujali pembe zake au ni nani tutamchukulia hatua kali zikiwamo za kisheria…hatuwezi kuendelea kwa mchezo huu” alisema Nape.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, amewaagiza viongozi wa vijiji waanze mara moja mchakato wa kuanzisha mfuko mpya na baada ya ngazi hiyo kukamilisha kazi hiyo ipelekwe kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kupata baraka zake ili uweze kuanza kazi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment