Mkuu
wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (katikati) akizungumza
katika Mdahalo wa Mara Bora kwa Uwekezaji na Kuishi, mjini Musoma. Wanaomsikiliza
kwa makini ni Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob (wa pili kushoto),
Katibu wa MRPC, Pendo Mwakyembe (kushoto), Katibu wa CCM Mkoa wa Mara,
Mjanakheri Ibrahim (kulia) na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo sehemu ya
Viwanda na Biashara, Gambaless Timotheo (wa pili kulia).
------------------------------------------------------
Na Christopher Gamaina, Musoma
----------------------------------------------
Mkuu
wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, waandishi wa habari
na wadau mbalimbali wa maendeleo wamejadili fursa za uwekezaji zilizopo
mkoani humo na kutaka msukumo wa kuzitangaza uongezwe ili zifahamike kwa
watu wengi ndani na nje ya Tanzania.
Hatua
hiyo ilifikiwa katika Mdahalo wa Mara Bora kwa Uwekezaji na Kuishi,
ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), na
kufanyika kwenye Hoteli ya MK mjini Musoma jana
Fursa
za uwekezaji zilizopo mkoani Mara zilizotajwa na kujadiliwa katika
mdahalo huo uliofana kwa aina yake, ni pamoja na ufugaji, uvuvi,
uchimbaji madini, utalii na kilimo cha mazao ya biashara na chakula. Sehemu ya waandishi wa habari walioshiriki mdahalo huo.
--------------------------------------------------
Katika
hotuba yake, mgeni rasmi RC Mtambi alisema mkoa wa Mara una utajiri wa
maliasili na rasilimali nyingi, lakini hazijatangazwa ipasavyo ili
kuwashawishi watu wengi kujitokeza kuwekeza kwenye biashara
zinazohusiana nazo.
Maliasili
na rasilimali hizo ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa
Victoria, madini aina ya dhahabu, mifugo na ardhi kubwa inayofaa kwa
kilimo cha mazao ya chakula na biashara - kama vile mahindi, ndizi,
kahawa, pamba, alizeti na viazi vitamu.
“Lakini
pia, tuna miradi mikubwa iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa na
serikali; tuna Uwanja wa Ndege Musoma, Hospitali ya Rufaa Kwangwa, Chuo
Kikuu cha Mwalimu Nyerere kule Butiama, na barabara zinaendelea
kuboreshwa katika mkoa mzima.
“Neema
hii tuliyo nayo katika mkoa wa Mara haijatangazwa vizuri. Ninawaomba
waandishi wa habari mtumie kalamu zenu kutangaza fursa hizi kwa
maendeleo ya mkoa wetu na Taifa kwa ujumla,” alisema RC Mtambi.
Kiongozi
huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuipongeza MRPC kwa kuandaa
mdahalo huo na kuanzisha mpango wa tuzo za kila mwaka kwa waandishi wa
habari wa mkoani Mara watakaokuwa wanafanya vizuri. Waandishi wa habari wakifuatilia mada katika mdahalo huo.
-----------------------------------------------
Awali,
Mwenyekiti wa MRPC, Mugini Jacob alimshukuru RC Mtambi kwa kukubali
kuwa mgeni rasmi, pamoja na wadau wa maendeleo walioitikia wito wa
kushiriki mdahalo huo.
Tuzo kwa waandishi
Kuhusu
tuzo kwa waandishi wa habari - zitakazojulikana kwa jina la Mara
Quality Journalism Awards, Jacob alisema zitaanza kutolewa Desemba mwaka
huu na kwamba washindi watazawadiwa vyeti na fedha taslimu.
“Tuzo
hizi zitakuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha uandishi bora (promoting
quality journalism), ambao pia unachangia kuufanya mkoa wa Mara kuwa
sehemu bora kwa uwekezaji na kuishi.
Alitaja
makundi ya habari zitakazohusika katika tuzo hizo kuwa ni kilimo,
ufugaji, madini, utalii, ujenzi na miundombinu, uhifadhi wa wanyamapori,
maji, uvuvi endelevelu (sustainable fishing) na makundi maalum ya
jamii.
“Tunaamini
uandishi bora, yaani quality journalism katika maeneo hayo utasaidia
kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongoza na Rais Dkt
Samia Suluhu Hassan katika kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Mara na
Taifa letu la Tanzania kwa ujumla,” alisema Jacob. Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa MRPC (kushoto) alimkabidhi RC Mtambi
zawadi ya kumkaribisha mkoani Mara, yenye picha yake na fursa za
uwekezaji zinazopatikana mkoani humo, iliyoandaliwa na klabu hiyo.
Mbali
na waandishi wa habari, baadhi ya wadau wa maendeleo wa mkoani Mara
walioshiriki katika mdahalo huo ni kutoka Mgodi wa Barrick North Mara,
Grumeti Reserves/ Grumeti Fund, HAIPPA PLC, Nyihita Sunflower, CCM,
TANROADS, TCCIA, WAMACU, Kampuni ya Swala na Benki ya Azania, miongoni
mwa wengine. Mkuu
wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, viongozi wa MRPC na wadau
mbalimbali wa maendeleo (wa nne kulia mbele) akiwa katika picha ya
pamoja mara baada ya kuhitimisha mdahalo huo. (Picha zote na Mara Online
News)