Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh Dkt Vicent Anney ametoa ngao za motisha kwa Wakuu wa shule za Sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mh. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi
Mhe. Mtambi alizitaka shule ambazo zimefanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha Nne mwaka 2023 kuhakikisha wanapewa ngao yenye kuwaongezea motisha zaidi ili waweze kuongeza juhudi katika ufundishaji wa watoto shuleni, na kwa zile shule ambazo hazikufanya vizuri pia, wakuu wa shule wapewe vinyago ambavyo wataviweka katika ofisi zao ili kuongeza motisha ya ufundishaji katika shule.
Kupitia hafla hiyo iliyofanyika tarehe 15 July 2024 ukumbi wa halmashauri ya mji wa Bunda, Mkuu wa Wilaya ya Bunda aliikabidhi shule ya sekondari Ikizu ngao ya ushindi na kutoa kinyago kwa sekondari Hunyari kwa kuburuza mkia kwa shule za halmashauri ya wilaya.
Akikabidhi tuzo hizo, Mhe. Anney alimshukuru Mh Mkuu wa mkoa wa Mara kwa kuwa na upendo kwa Walimu na kupendekeza wazo hilo litakalosaidia kuinua kiwango cha ufaulu
"Hii ilikuwa ni ajenda yangu ya kwanza tangu nilipofika katika Wilaya hii ya Bunda, Elimu ni fursa, Elimu ni chombo cha ukombozi na Elimu inamfanya mtu kuishi na kwenda eneo lolote Duniani, leo hii tupo hapa kwa ajili ya kutoa motisha chanya kwa shule zilizofanya vizuri kwa kutoa ngao ya pongezi na shule zilizofanya vibaya pia tutawapa kinyago ili kuongeza motisha zaidi katika ufundishaji wa watoto shuleni." Alisema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Ndugu George S Mbilinyi alisema Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inajumla ya shule za Sekondari 26, mbili zikiwa ni za binafsi na 24 za serikali.
" Tunampongeza Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa kuweza kutimiza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mara la kuwataka tuwapatie motisha hizi wakuu wa shule za sekondari kwa waliofanya vizuri na waliofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha Nne 2023". Alisema Mbilinyi
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Bi. Nambua Semlugu amesema "tunatakiwa tusimamie vizuri suala la lishe na utoro shuleni, hii itapunguza idadi ya wanafunzi shuleni kufeli na itaongeza umakini zaidi darasani.
" Binafsi tukio hili linatarajia kuleta matokeo mazuri katika shule zetu, kwa niaba ya Walimu tunaahidi kuwajibika kwa kuhakikisha tunaongeza juhudi zaidi, ombi langu ni kwamba, vinyago vinavyoletwa katika shule zilizofanya vibaya, visiwe vya Wakuu wa shule pekee ama shule pekee bali, viwe vya jamii nzima." Alisema Majura.
0 comments:
Post a Comment