JESHI la Polisi nchini limemvua madaraka ya ukuu wa Polisi wa Wilaya ya Serengeti, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Paulo Mng’ong’o, wakati Ofisa Usalama wa Wilaya hiyo Said Mussa, akishughulikiwa na viongozi wake kwa mujibu wa taratibu za ajira yake.
Inadaiwa maofisa hao wawili walikamatwa na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boaz, alisema Machi 23 saa tano asubuhi maofisa hao wakiwa na gari la Polisi namba PT 1862 walikutwa na askari hao katika eneo la Mlimafedha hifadhini humo.
Kamanda Boaz alisema baada ya maofisa hao kuhojiwa walidai wanafuatilia taarifa za ujangili katika eneo hilo ambapo maelezo hayo yaliwatia shaka askari na maofisa wa hifadhi hiyo na hivyo kuondoka nao hadi ofisini kwa Mhifadhi Mkuu kwa mahojiano zaidi.
“Waliwatilia shaka kwa kuwa hapakuwa na taarifa za kuwapo eneo hilo kwa maofisa hao na shughuli wanayodai kuifanya … wakati wanaondoka na maofisa hao walibakiza askari wa doria eneo hilo lenye mashimo mengi ya migodi,” alisema Kamanda Boaz.
Alisema saa 7 mchana watu watano walitoka ndani ya shimo jirani na lilipokuwa limeegesha gari la Polisi ndipo askari hao wa doria walipowakamata wakiwa na viroba tupu na vingine tisa vikiwa na mawe yaliyochimbwa kutoka shimoni humo na zana za kuchimbia na mashine ya kupimia vyuma.
Kamanda Boaz aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Maiga Majanjala (26) wa Nyamakokoto, Bunda; Jonas Marwa (42); Alex Mabu (29) ambaye ni mwalimu wa Sekondari ya Kambarage; Mniko Nyamhanga (30), Mwita Kinyeti (33) wote wakazi wa Mugumu, Serengeti.
“Watuhumiwa hao watano waliokamatwa wamefikishwa mahakamani leo (jana) kujibu mashitaka yakiwamo ya kuingia hifadhini bila kibali na kuchimba madini ndani ya hifadhi kinyume cha sheria,” alisema Kamanda Boaz.
Kutokana na tuhuma hizo nzito kulikumba Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa liliundwa jopo la wapelelezi kutoka taasisi zinazohusika na jambo hilo ili kuchunguza pamoja na mambo mengine, uhalali wa maofisa hao kuingia hifadhini bila kutaarifu mamlaka husika.
“Kwa upande wa maofisa wanaotuhumiwa pamoja na dereva wa gari hilo Koplo Phillimatus, hatua za kinidhamu zitachukuliwa na kanuni za ajira zao zimeanza kuchukuliwa,” alisema Kamanda Boaz. Uchunguzi ukikamilika, nao watafikishwa mahakamani kwa kukutwa katika hifadhi hiyo ya Taifa bila kibali, aliongeza Kamanda Boaz.
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment