na Berensi Alikadi, Bunda
WANANCHI wilayani Bunda mkoani Mara wamempongeza Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha kundi la vijana Mkoa wa Mara, Ester Bulaya (CCM) kwa msimamo wake wa kuchangia hoja mbalimbali bungeni ikiwa ni pamoja na matatizo ya wananchi wa Bunda.
Walitoa pongezi hizo jana kwa nyakati tofauti mara baada ya kusikia taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa mbunge wa Jimbo la Bunda, Steven Wasira (CCM) alimkoromea Bulaya kwa madai ya kuikosoa bajeti na hatua yake ya kuyazungumzia masuala ya Bunda wakati yeye si mbunge wa jimbo hilo.
Nyamhanga Maswi mkazi wa Tairo alisema Ester ni mbunge wa Mkoa wa Mara ambaye anawakilisha wananchi hususani kundi la vijana ambalo ndilo linaathirika zaidi ambao Wasira ameshindwa kuwasaidia kwa muda wote akiwa madarakani licha ya kuwadanganya waunde vikundi ili wapate mikopo lakini hakuna alichowatimizia.
“Sisi wana Bunda tunampongeza sana huyu mbunge maana tangu amechaguliwa amekuwa akichangia hoja nyingi zinazogusa maendeleo yetu na hii inaonyesha ni jinsi gani anavyokerwa na maisha duni waliyonayo wananchi wa Mkoa wa Mara tumeona juhudi zake hususan katika suala la wananchi wa Tairo ambao maeneo yao yamechukuliwa na EPZ lakini hawajalipwa…’’ alisema.
Naye Boniface Noni wa mkazi wa Bunda alisema wananchi wana imani kubwa na mbunge huyo (Bulaya) na kwamba yeye kama mbunge anao wajibu wa kuipinga bajeti kama ameona haifai na wala haiwalengi wananchi anaowawakilisha hivyo alichofanya ni sahihi na wala hapangiwi na mbunge mwingine kitu cha kuongea.
Naye Abubakari Kiharata wa Kijiji cha Maliwanda alieleza kusikitishwa na kitendo cha Wasira kumwingilia mbunge huyo katika majukumu yake ya kikazi na kudai kuwa hapaswi kuuliza wala kuzungumzia mambo ya Bunda kwa madai kuwa hilo ni jimbo lake jambo ambalo wananchi hao wamelipinga na kusema kuwa jimbo analoliongoza Wasira ni mali ya wananchi yeye ameshindwa kuwaomgoza awaachie wenzake
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment