Na Shomari Binda, Musoma,
Watoto watatu wa familia moja wamewafikisha wazazi wao katika kituo kikuu cha Polisi Mjini Musoma kitengo cha dawati la jinsia wakidai kutelekezwa na kuwafanya kuishi maisha ya kutangatanga mitaani ili hali wazazi wao wakiwepo na kuendelea na maisha ya kila siku bila kujua wao wanaishi vipi.
Akiongea na mwandishi wetu nje ya kituo hicho cha Polisi, mmoja wa watoto hao aliyejitambulisha kwa jina la Justine Kichere alisema baba yao mzazi kwa kushirikiana na mama yao wa kambo ambaye hawakuweza kumtaja jina lake waliwafukuza nyumbani kwa kuwatupia nguo zao kwa kile walichokieleza kudaiwa kuwa (machokoraa) watoto wa mitaani.
Wakielezea chanzo cha tukio hilo la kufukuzwa nyumbani,Justine mwenye umri wa miaka 14 mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Rwamlimi A iliyopo Manispaa ya Musoma alisema waliitwa na mama yao wa kambo akiwa na wadogo zake wawili James Kichere mwenye umri wa miaka 13 na Gerald kichere mwenye umri wa miaka 12 na kuelezwa kuwa mama yao anaumwa na amelazwa katika hospitali ya Mkoa hivyo kuwataka kwenda kumsalimia mama yao.
Mtoto huyo alieleza kuwa wakiwa njiani kuelekea hospitalini huku wakiwa hawapajui waliomba msaada katika gari moja nakueleza wanakwenda katika hospitali ya Mkoa na kupandishwa kisha kuelekea wasipokujua na walipofika na kuuliza waliambiwa wapo maeneo ya Ramadi.
Alidai baada ya kudaiwa kupotea waliomba msaada wa kurudi nyumbani Musoma na kusaidiwa lakini mara baada ya kufika nyumbani bila kuulizwa kilichowasibu walitupiwa nguo zao nje na kutakiwa kuondoka nyumbani na watafute mahala pengine watakapo kwenda kuishi.
Justine alisema baada ya kufukuzwa na baba yao pamoja na mama yao wa kambo waliamua kwenda kwa mama yao ambaye alitengana na baba yao anayeishi maeneo ya Baruti na kukaa kwa muda wa siku mbili kisha mama yao kuwataka kurudi kwa baba yao kwa kuwaeleza kuwa hana pesa ya kuwalisha wote watatu.
Aliendelea kueleza baada ya kuona hawana sehemu ya kwenda waliamua kutaka kuingia katika maisha ya mtaanii na waliishi katika maisha hayo kwa muda wa wiki moja huku wakiwa wakilala katika jumba bovu maeneo ya Nyakato na kuyaona maisha hayo hawayawezi na kuamua kwenda kituo cha Polisi ili kuweza kupata msaada zaidi.
Mtoto huyo aliongeza kuwa hilo sio tukio la kwanza kwa baba yao Kichere Sangi aliyemueleza kuwa ni mfanyabiashara wa duka la rejareja katika maeneo ya Kigera kufanya hivyo kwa kuwa alishawahi kumfukuza kaka yao Geofrey Kichere aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika shule ya sekondari Bweri ambaye mpaka sasa hajulikani halipo.
Aidha watoto hao walisema lengo la kwenda katika kituo cha Polisi ni kutaka kupata msaada kwa kuwa maisha wanayoishi mtaani ni magumu na wameshindwa kwenda shuleni huku mmoja wao akiwa anakabiliwa na mtihani wa darasa la saba
Mwandishi wetu alifika katika ofisi ya dawati la jinsia katika kituo cha Polisi Musoma kutaka kujua hatima ya watoto hao na kuelezwa kuwa wanazotaarifa hizo na hatua waliyochukua ni kundika barua wa wito kwa wazazi ili kuelezea madai ya watoto hao.
0 comments:
Post a Comment