Home » » MUSOMA KUONDOKANA NA KERO YA MAJI KARIBUNI

MUSOMA KUONDOKANA NA KERO YA MAJI KARIBUNI



na Sitta Tumma, Musoma
MJI wa Musoma unatarajia kuondokana na tatizo la maji kutokana na mradi wa maji safi na salama unaotarajiwa kuanza kujengwa Desemba mwaka huu.
Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), aliiambia Tanzania Daima juzi mjini hapa kwamba, mradi huo ukakaogharimu zaidi ya sh bilioni 50, umelenga kumaliza kama si kupunguza adha ya maji safi ya kunywa iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu wananchi wa jimbo hilo.
Alisema mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa, na utekelezwaji wake umepangwa kutumia miezi 18 kuanzia Desemba mwaka huu.
Mradi huu ni mkubwa na utekelezwaji wake utaanza rasmi Desemba mwaka huu, lengo langu ni kuhakikisha wananchi wa Musoma wanaondokana na tatizo la maji lililokuwa likiwasumbua kwa miaka mingi.
“Jitihada ninazozifanya mimi binafsi pamoja na serikali ni kuhakikisha tatizo la maji na sekta nyingine zinapatiwa ufumbuzi kwa faida ya wananchi. Naishukuru Ufaransa kwa kukubali kutufadhili sh bilioni 50 kwa ajili ya kutatua kero ya maji hapa Musoma mjini.
"Wakati naomba kura mwaka 2010 niliwaahidi wananchi kuwapatia maendeleo ya kisekta. Kwa hiyo kazi niliyonayo ni kuhakikisha Musoma inakuwa na maendeleo makubwa tofauti na miaka ya nyuma, maana nia ninayo, uwezo ninao na sababu ninazo za kuijenga Musoma kimaendeleo. Ninachoomba kwa wananchi wangu waendelee kutupatia ushirikiano mimi na madiwani wa manispaa yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, aliwaambia wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), kilichofanyika mwishoni mwa wiki kuwa mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Musoma, kwani utakuwa suluhisho la kero ya maji.
Alisema mbali na mradi huo, amefanikiwa kupata ufadhili mwingine wa visima vya maji safi na salama kutoka kwa mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Mustafa Sabodo.
Nyerere alimpongeza Sabodo kwa dhamira yake nzuri ya kusaidia Watanzania wakiwemo wananchi wa jimbo lake, hivyo aliwaomba Watanzania wote waendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu mfanyabiashara huyo kwa michango yake mizuri ya kujenga taifa
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa