Home » » UWEKEZAJI BARRICK WALETA MANUFAA - SERIKALI

UWEKEZAJI BARRICK WALETA MANUFAA - SERIKALI



na Mwandishi wetu, Tarime
SERIKALI imeipongeza Kampuni ya African Barrick Gold (ABG) kwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na migodi yake nchini katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, baada ya kufanya ziara ya mgodi huo uliopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Katika ziara hiyo, Masele pamoja na Naibu Waziri wa Nchi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, walitembelea miradi mikubwa ya jamii ambayo inatekelezwa na mgodi huo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, maji na afya.
Masele alisema mgodi wa North Mara kihistoria umekuwa na matatizo ya mahusiano na jamii inayoizunguka, lakini hatua kubwa zimepigwa sasa kuboresha mahusiano na vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
“Mimi binafsi Bungeni nimesikia pale wabunge wa huku wakilalamika kwamba kuna shule za msingi ziko jirani sana na mgodi. Kazi za mgodi zinapoendelea, ile milipuko inakuwa ikiwaathiri wanafunzi.
“Lakini leo nimetembelea shule ambayo inatakiwa kujengwa ili kuhamisha ile ambayo inaathiriwa na shughuli za mgodi. Nimejionea kazi ambayo inaendelea pale. Wakandarasi wako saiti wanajenga hizo shule.”
Masele alisema kuwa kipindi cha nyuma kulikuwa na tatizo la wanafunzi kukaa chini katika shule zilizopo katika maeneo hayo ya mgodi, lakini mgodi wa North Mara sasa unatekeleza mradi kabambe wa kuzipatia shule hizo madawati.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa ABG wa shughuli za shirika, Deo Mwanyika, alisema mgodi wa North Mara umeingia mkataba na vijiji vyote vinavyouzunguka wa kuwekeza zaidi ya dola milioni 8.5 (zaidi ya sh bilioni 13) kwenye miradi mbalimbali ya jamii ikiwemo kwenye sekta za elimu, afya na maji.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa