Home » » Posho yawatesa madiwani, wazuia Mwenge wa Uhuru

Posho yawatesa madiwani, wazuia Mwenge wa Uhuru

KATIKA hali isiyo ya kawaida, madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, juzi waliamua kufunga geti la halmashauri hiyo, kwa kile walichodai hawawezi kwenda kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, bila kulipwa posho zao.
Sakata hilo ambalo MTANZANIA ililishuhudia, lilianza saa 2 subuhi, hali iliyopelekea Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kuamua kuondoka na kumuacha Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, wakuu wa idara pamoja na watumishi wakiwa wamepigwa na butwaa.

Gazeti hili lilimshuhudia, Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma na Diwani wa Kata ya Mwisenge, Bwire Nyamwelo (CHADEMA), akiwa amesimama katika geti la halmashauri hiyo, huku mlinzi akiwa pembeni na kuzuia magari kutokuondoka hadi pale watakapolipwa posho.

"Hatuwezi kukubaliana na hali ya kudharauliwa, sisi kama madiwani, hatuwezi kupelekwa kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, tukiwa kwenye magari yasiyo ya manispaa, suala la posho lazima lishughulikiwe.

"Inakuaje mnatupatia gari la Chama cha Walimu (CWT), wakati tuna magari yetu, hatuwezi kwenda huko hadi mambo haya tunayoyataka yatakaposhughulikiwa, tutatumiaje magari ya kuazima wakati tuna magari yetu, hili haliwezekani na posho lazima tupewe kwanza," alisikika Naibu Meya huyo.

Alipoulizwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Ahmed Sawa alisema ameshangazwa na uamuzi wa madiwani hao.

"Nasikia Mwenge umeshafika eneo la mapokezi kutoka Butiama, lakini bado geti limefungwa kiukweli kwa sasa sina la kuzungumzia kuhusiana na tukio hili ila ngoja tuone hali itakavyokuwa, kama wataendelea kuwa na msimamo wao.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Chrisant Nyakitita alilaani kitendo hicho na kukiita ni utovu wa nidhamu.

Katika mbio hizo, miradi ya maendeleo 17, inatarajiwa kuzinduliwa yenye thamani ya Sh milioni 904,041,293.

chanzo: MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa