WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zikiwa zimeanza rasmi
jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemuweka chini ya
ulinzi Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyasura, Wilaya ya Bunda mkoani Mara,
John Yapanda, baada ya kiongozi huyo kumnyang’anya kadi ya kupigia kura
mgombea wa udiwani kata hiyo, Julius Wassira (CHADEMA).
Ofisa Mtendaji huyo wa kata alifika kwenye mkutano wa uzinduzi wa
kampeni wa CHADEMA katika kata hiyo, kisha kumwamuru Wassira amkabidhi
kitambulisho chake cha kupigia kura, kwa madai amewekewa pingamizi na
mmoja wa wagombea wa vyama vingine.
Baada ya Wassira kumpa kadi yake hiyo, Yapanda alitaka kuondoka
nayo, jambo lililosababisha baadhi ya viongozi, wapenzi na makada wa
chama hicho kuchachamaa na kumkamata mtendaji huyo.
Baada ya Ofisa Mtendaji huyo kukamatwa, umati mkubwa wa wananchi
uliokuwa umehudhuria mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni, nao
walichachamaa wakitaka kuanza kumsulubu, lakini busara za viongozi wa
CHADEMA zilitumika kwa kutuliza munkari wao.
Hata hivyo, baadaye mtendaji Yapanda alipandishwa jukwaani na
kuamuriwa aeleze sababu za kumnyang’anya mgombea wao kadi ya kupigia
kura, ambapo alisema: “Jamani sina nia mbaya mimi, kuna pingamizi
amewekewa kwa kutumia jina la Wassira eti siyo lake.”
Akihutubia mkutano huo, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere,
alisema Serikali ya CCM imeshindwa kuwasaidia wananchi kuondokana na
umaskini.
Alisema CCM na viongozi wake wamewatelekeza wananchi na kushindwa
kuwapatia huduma bora za kibinadamu kama vile maji, afya, barabara na
elimu bora, hivyo aliwaomba kumchagua mgombea wa CHADEMA, Wassira kuwa
diwani wao ili awatumikie kwa kuwapatia maendeleo
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment