Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katika hukumu yake ya Julai 31, 2013 iliyotolewa na Hakimu Kahimba, kila
mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani kwa kila kosa
na adhabu zote kwenda pamoja.
Wakati Serikali na wadau mbalimbali wakipiga kelele kuhusu
kukithiri kwa ujangili unaotishia kutoweka kwa wanyamapori nchini,
baadhi ya mahakimu wamebainika kutoa hukumu zinazokinzana na Sheria ya
Wanyamapori namba 5 ya 2009 na ile ya makosa ya uhujumu uchumi.
Baadhi ya hukumu dhidi ya makosa hayo zinatolewa
kinyume na sheria, hivyo kuwapo tafsiri kwamba mhimili huo wa utoaji wa
haki ni moja ya maeneo ambayo watumishi wake wanajihusisha na vitendo
vya rushwa, kama ambavyo imethibitishwa na matokeo ya tafiti mbalimbali.
Uchunguzi kuhusu mwenendo wa kesi za uhujumu
uchumi katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, umebaini
mahakama hiyo kutoa hukumu kadhaa zinazokinzana na sheria husika.
Mojawapo ya hukumu hizo ni ile iliyotolewa katika
shauri namba Eco.119/2012, ambapo mshtakiwa Kision Joseph Masanja na
wenzake walitiwa hatiani katika makosa matatu baada ya kukiri mbele ya
mahakama.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Amon Kahimba,
watuhumiwa hao walishtakiwa kwa kuingia ndani ya hifadhi, kukutwa na
silaha ambazo ni panga na kisu. Shtaka la pili ni kukutwa na nyaya tatu
za kunasia wanyama na la tatu ni kukutwa na mguu na kichwa cha mnyama
aina ya pofu, vyenye thamani ya Sh2.55 milioni bila kibali.
Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa Julai 29, 2013,
watuhumiwa hao baada ya kutiwa hatiani, walihukumiwa kifungo ama cha
miezi 18 jela au kulipa faini ya Sh100,000 kwa kila kosa.
Katika kesi ya pili namba Eco.55/2011, gazeti hili
lilibaini kuwa mbele ya hakimu huyo, mshtakiwa Sai Masuka na wenzake
watatu walitiwa hatiani baada ya kukiri makosa matatu yaliyokuwa
yakiwakabili.
Makosa hayo ni kuingia hifadhini bila kibali,
kukutwa na silaha za jadi; pinde mbili, mkuki, mishale mitatu, panga,
visu viwili. Katika shtaka la tatu walikutwa na vipande vinne vya nyama
ya nyumbu, pembe ya pofu na mikia 13 ya nyumbu vyote vikiwa na thamani
ya Sh6.2 milioni.
Katika hukumu yake ya Julai 31, 2013 iliyotolewa
na Hakimu Kahimba, kila mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miezi miwili
gerezani kwa kila kosa na adhabu zote kwenda pamoja.
Kwa mujibu wa sheria hizo, makosa ya kuingia na
kukutwa na silaha za jadi hifadhini huchukuliwa kama makosa ya jinai,
lakini watuhumiwa wanapokutwa na nyara aina yoyote na silaha za kivita,
makosa hayo huangukia kwenye kesi za uhujumu uchumi.
Kwa maana hiyo, uamuzi wa Hakimu Kahimba
unakinzana na vifungu 86 (1) na (2) (ii) vya Sheria ya Hifadhi ya
Wanyamapori namba 5 ya 2009 ikisomwa sambamba na aya ya 14 (d) katika
jedwali la kwanza na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya sheria ya uhujumu
uchumi sura 200 (RE:2002).
Kwa mujibu wa vifungu hivyo, washtakiwa baada ya
kutiwa hatiani walipaswa kutumikia kifungo kisichopungua miaka 20
gerezani lakini kisichozidi miaka 30; na mahakama kwa nyongeza, inaweza
kuweka faini isiyozidi Sh5 milioni au faini ambayo ni mara kumi ya
thamani ya nyara ambazo washtakiwa walishtakiwa nazo.
Hata hivyo, Hakimu Kahimba alipohojiwa alisema madai
yanayotolewa kwamba hukumu hizo hazikidhi matakwa ya sheria hayana
msingi na kwamba amekuwa akitoa adhabu kubwa kuliko zile zinazobainishwa
na sheria.
“Kwanza sheria ina upungufu mkubwa....lakini bado
tunatoa hukumu kali sana ambazo ni zaidi ya zilizotajwa kwenye Sheria
namba 5 ya Wanyamapori ya 2009,” alisema hakimu huyo.
Alisema washtakiwa wengi hukaa mahabusu muda
mrefu, kuanzia mwaka mmoja au zaidi kutokana na majalada kuchelewa
kupata ruhusa ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, wengine kukosa
wadhamini wenye sifa.
“Asilimia 99 ya kesi zilizopo mahakamani hapa ni
za nyara, majalada huchukua muda mrefu kuletwa....wengi wanakuwa
mahabusu kwa muda mrefu... haki zao za msingi huzingatiwa wakati wa
hukumu,” alisisitiza Kahimba.
Waendesha Mashtaka
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi, Mkoa wa Mara,
Lukelo Samuel alikiri kupokea malalamiko ya kesi zinazotolewa hukumu
kinyume na sheria.
“Kuna matatizo makubwa kwenye mahakama
zetu....sheria ziko wazi lakini uamuzi unaotolewa ni kinyume chake.
Malalamiko hayo yapo na tunayafanyia kazi,” alisema Samuel.
Alisema katika hatua za awali wamelazimika
kuhamishia baadhi ya kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara,
pale walipobaini mapema kuwapo kwa dalili za ukiukwaji wa sheria.
Wakili Juma Thomas alisema iwapo hukumu
zingezingatia mahitaji ya sheria husika, wakosaji wangejifunza, kujuta
na kuwa fundisho kwa watu wengine lakini kinyume chake uamuzi wa aina
hiyo unashawishi ujangili kuongezeka.
“Kwenda kinyume na hitaji la sheria ni kichocheo
cha ongezeko la ujangili....pia kunakuwa na dalili ya rushwa, maana
sheria iko wazi...imeainisha adhabu. Ukienda nje ya hiyo lazima kuna
kilichokusukuma, kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye vyombo vya uamuzi,
juhudi zote za Serikali hazina maana,” anasema.
Kwa upande wake, Cosmas Tuthuru ambaye ni Wakili
wa Mahakama Kuu alisema Serikali inapaswa kukata rufaa pale mahakama za
chini zinapotoa hukumu zinazokinzana na sheria ili kutokutoa mwanya wa
kuongezeka kwa vitendo vya ujangili.
“Jamhuri kwa hili inatakiwa kulalamikia uamuzi
kama huu unaotolewa kinyume cha sheria za uhujumu uchumi na ile ya
wanyamapori, lakini cha kushangaza hawakati rufaa...kisheria usipokata
rufaa uamuzi unabaki kama ulivyo....hawana haja ya kuendelea kulalamikia
ongezeko la ujangili wakati hawachukui hatua,” alisema Tuthuru.
Kwa kipindi kirefu kumekuwa na madai ya baadhi ya mahakama kutekwa na mtandao wa ujangili, hivyo kusababisha watuhumiwa wengi kuachiwa na wengine wanaotiwa hatiani kupewa adhabu ndogo kinyume cha sheria
Chanzo;Mwananchi
Kwa kipindi kirefu kumekuwa na madai ya baadhi ya mahakama kutekwa na mtandao wa ujangili, hivyo kusababisha watuhumiwa wengi kuachiwa na wengine wanaotiwa hatiani kupewa adhabu ndogo kinyume cha sheria
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment