Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Panya mzee akiwa mwenye nguvu baada ya kuwekewa damu changa
Watu wengi wangetamani kuona hawazeeki, wanabakia na nguvu za ujana na kwa sababu hiyo wanasayansi wanatafiti kupata ufumbuzi.
Vyuo vikuu vitatu maarufu duniani vimekuja na
matokeo ya utafiti ambao unaweza kukata kiu ya wengi ambao hawatamani
kamwe kuzeeka.
Siku hizi kumekuwapo na usemi kuwa uzee mwisho
Chalinze, jijini (Dar es Salaam) kila mtu ‘baby’ (mtoto). Hii ikiashiria
watu hawapendwi kuitwa wazee ingawa umri wao ni mkubwa.
Wamekuwa na kauli hiyo ili kulazimisha mazingira
kwamba bado wana uwezo wa kufanya yote kama wenye damu changa lakini
katika uhalisia si kweli.
Utafiti wa vyuo vya Harvard na California vya
nchini Marekani vikishirikiana na Cambridge nchini Uingereza, unajenga
mazingira ya kuifanya ndoto ya wenye mawazo ya kuukataa uzee kuwa kweli.
Watafiti hao walichukua damu ya panya mchanga na
kumuingizia kwa aliyezeeka. Walichobaini ni kwamba panya yule mzee
alichangamka na kurejewa na nguvu za ujana.
Matokeo ya utafiti huo yanatoa mwanya kwa wanasayansi kukaa kitako na kutengeneza dawa ambayo mtu akitumia anaweza kutozeeka.
Kutozeeka huko ni kuendelea kuwa na dalili za
ujana kama vile kutokuwa na makunyanzi usoni na viungo kuendelea kuwa na
nguvu ya kutekeleza mambo yote kama kawaida hata wenye umri wa zaidi ya
miaka 70.
Utafiti ulivyofanyika
Timu ya watafiti hao wiki hii walitangaza kuwa
wamegundua namna ambayo wanaweza kumfanya panya mzee kutokuwa na dalili
zinazofanana na umri huo.
Wanasema kwenye utafiti huo kuwa mara baada ya
kuchukua damu ya panya mchanga na kumuingizia aliyezeeka ghafla
alibadilika na kurejewa na nguvu zilizomfanya achangamke na kutenda kama
vile bado hajazeeka.
Walichobaini ni kwamba ile damu ilienda
kuchangamsha ubongo kiutendaji na kuwezesha kuimarika kwa utendaji wa
mwili kwa jumla.Kwa kawaida mambo yote yanayotendeka mwilini huongozwa
na ubongo kwa kuhamasisha homoni fulani kulingana na jambo husika.
Wanasema kwenye damu ya panya mdogo kuna aina ya protini ijulikanayo kama GDF11, ambayo wanahisi ndiyo iliyochochea jambo hilo.
Wakasema wanachofanya ni kuchunguza kama hii protini ndiyo inayochochea ujana.
Mtaalamu wa Tanzania
Akizungumzia juu ya utafiti huo, mtaalamu wa Afya
ya Jamii katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk Alex Mwita anasema
hakuna haja ya watu kujipa matumaini kutokana na ugunduzi huo kwa sababu
hadi kupatikana dawa itakayotumika kwa binadamu inaweza kuchukua miaka
zaidi ya 10.
“Huu ni ugunduzi kwa panya. Hadi kufikia mafanikio kwa binadamu, ni utafiti utakaochukua miaka mingi,” anaonya Dk Mwita.
Alisema zipo tafiti nyingi kuhusukile
kinachosababisha uzee na kujaribu kutafuta njia za kuuzuia lakini bado
mafanikio hayajapatikana.
Nini kinasababisha uzee
Wataalamu wanasema kuwa ni jambo ambalo liko wazi kwamba uzee unapozidi, mwili hushindwa kujimudu na hatimaye kusababisha kifo.
Utafiti uliosimamiwa na mtaalamu wa Elimu ya
Viumbe katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani, Dk John Langmore
ulibaini kuwa mtu anakufa kwa umri kutokana na viungo vya mwili
kushindwa kutekeleza kazi zake kikamilifu.
Hali hiyo inachangiwa na kasi ya seli za mwili kuzaliana kupungua kwa kiwango kilichopindukia huku zinazokufa zikiwa nyingi.
Mfumo huo uko hivi, mtoto anapozaliwa ukuaji wake
ni wa kasi sana. Hii inatokana na uwiano wa seli zinazokufa kuwa kidogo
zaidi ukilinganisha na zile zinazozalishwa.
Uwiano wa seli zinazokufa na zinazozalishwa hufikia mahali ukalingana. Ikifikia kiwango hicho mtu huwa hakui tena.
Uzee unaanza pale uwiano wa seli zinazokufa kuwa wa juu zaidi kuliko zile zinazozalishwa.
Hali hiyo huanza kuusababisha mwili kusinyaa na kusababisha mikunjo sehemu mbalimbali za mwili.
Kasi ya seli zinazokufa ukilinganisha na
zinazozaliwa huendelea kuongezeka na hali hiyo huendelea kuongeza
makunyanzi na hata baadhi ya viungo kupoteza uwezo wake wa kawaida.
Kinachosababisha seli kutozaliana
Dk Langmore na timu yake wanaamini kufa kwa seli
ni jambo la kawaida lakini sababu ya kasi ya kuzaliana kupungua
kulingana na umri, ni jambo muhimu pia.
Waliamini ufumbuzi huo ndiyo utakaowapa sababu ya mtu kuzeeka na pingine kutafuta namna ya kuzuia uzee.
Walibaini kuwa DNA ndani ya seli ndiyo inayohusika katika kuwezesha seli kuzaliana au kutozaliana.
Wakabaini kuwa ina kichocheo ambacho kinasababisha mazingira hayo ya seli kutozaliana hasa mtu anapofikia umri mkubwa.
Dk Mwita anasema kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuna kitu kinachojulikana kisayansi kama Telomere.
Anasema Telomere inauhusiana na seli kudumu muda
mrefu ikiwa na uwezo wa kuzaliana au la. “Telomere ni kama kamba ya
kufunga viatu. Inapomalizika unakua mwisho wa seli kuendelea kuzaliana,”
anasema Dk Mwita.
Anafafanua kuwa watu wanaokuwa na Telomere ndefu ndiyo wanaishi muda mrefu na wale wanaokuwa na fupi, maisha nayo yanapungua.
Mtafiti mwingine wa Marekani, Dk Ronald Klatz
anaonya wanasayansi kutojikita tu katika kuchunguza sababu za uzee kwa
kutumia jeni na mfumo wa seli za mwili.
Akasema ipo haja pia kuchunguza mienendo ya mwili unavyoguswa na namna za ulaji, mazingira na misongo ya mawazo.
Akasema hali hizo kwa namna moja au nyingine zinachangia mwili kuchoka na hata kupunguza kiwango cha kawaida cha mtu kuishi.
Chanza:Mwananchi
Chanza:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment