Home » » BAWACHA WAMSHUGHULIKIA AIRO RORYA

BAWACHA WAMSHUGHULIKIA AIRO RORYA

Mbunge wa Rorya, Lameck Airo
BARAZA la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), limemshukia Mbunge wa Rorya, Lameck Airo jimboni kwake na kuwaeleza wananchi wake kuwa mbunge huyo haudhurii vikao vya bunge ipasavyo, ambako amehudhuria mara moja tu kikao cha kamati za bunge tokea achaguliwe 2015.
Hayo yalisemwa juzi kwa nyakati tofauti na Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao, wakati akiwahutubia wananchi wa Rorya kwenye viwanja vya Utegi na Shirati Obwere, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya viongozi wakuu wa BAWACHA kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki na Magharibi.
Alisema kuwa, amekuwa kwenye kamati mbili tofauti za bunge na mbunge Airo tokea waingie bungeni 2010, lakini amehudhuria vikao mara moja tu, jambo alilodai kuwa amejikita kwenye biashara zake kuliko masuala ya uwakilishi.
“Wana Rorya mimi nimekuwa na mbunge wenu kwenye kamati mbili tofauti, kwanza nilikuwa naye kamati ya bunge ya viwanda na biashara, kwa miaka miwili na nusu alihudhuria kikao mara moja…
“Sasa niko naye kwenye Kamati ya Ukimwi na Udhibiti wa Madawa ya Kulevya,  hajawahi kuhudhuria kikao hata kimoja, sasa huyu anawawakilisha vipi wakati haji kwenye vikao,” alihoji Abwao.
Aliwataka wananchi hao kuhakikisha hawarudii makosa kwenye chaguzi zijazo, wahakikishe wanachagua watu makini kwa ajili ya kuwawakilisha kwenye vikao vinavyofanya maamuzi juu ya mustakabali wa maisha yao huku akiwahakikishia watu wenye sifa wako CHADEMA.
“Mnasema toka ameingia madarakani hajawapa taarifa ya matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo, sasa akija mwambieni awape fedha hizo zijenge maabara,” alisema Abwao huku akishangiliwa na wananchi.
 Kiwelu adai Airo hata bungeni haonekani
Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kiwelu, aliwaeleza wananchi hao kuwa mbunge wao Airo, hata kwenye vikao vya kawaida vya bunge huwa haudhurii na hata akihudhuria huwa mtu wa kuunga mkono hoja hata zisizo na maslahi na wananchi hao.
Alisema kuwa, wabunge wengi wa CCM huwa hawawajibiki kwa wananchi walio wachagua kwa kuwa wanajua muda wa uchaguzi ukifika watawapa kofia, tisheti, khanga, pilau na nyama, jambo alilowataka wananchi hao kukataa udhalilishaji huo.
 Meya Musoma alia na wavamizi ardhi za wananchi
Meya wa Musoma Mjini, Alex Malima, alisema kuwa kumekuwa na tatizo la viongozi wa CCM na watu wenye fedha kuvamia maeneo ya wazi, jambo alilosema njia pekee ya kukomesha matukio hayo ni kuchagua viongozi waadilifu wanaosimamishwa na CHADEMA kuanzia ngazi za chini mpaka Taifa.
Aliwataka wananchi hao, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa kuanzia Novemba 23 mpaka 29 mwaka huu.
Alisema kuwa, wahakikishe wanapata wawakilishi wengi kwenye baraza la mamlaka la mji mdogo wa Shirati, ili waondokane na michango ya manyanyaso.
“Mimi ni Meya wa Musoma, CHADEMA tunaongoza halmashauri kule, hatuchangishi hii michango ya maabara, tumehakikisha kodi ya serikali inatumika na si kuwanyonya wananchi wetu,” alisema Meya Malima.
 Shirati walia 25,000 wanazotozwa ujenzi wa maabara
Mwenyekiti wa CHADEMA Rorya, Odero Odero, alisema kuwa wananchi wamekuwa wakichukuliwa mifugo yao pindi wanaposhindwa kulipa michango ya ujenzi wa maabara sh 25,000 jambo alilotaka Serikali kuacha ukandamizaji huo.
“Sijaitwa kwenye kikao chochote kujadili wananchi wachangie ujenzi wa maabara, wala hakuna kumbukumbu yoyote kwenye halmashauri yetu inayoonyesha kuwa tumejadili au kupitisha michango hii, hivyo hatuwezi kuchangia vitu tusivyojua vimeamriwa wapi na nani,” alisema diwani wa Nkoma, Lazaro Kitori, (CHADEMA)
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa