Dar es Salaam. Mjane wa Baba wa Taifa, Mama
Maria Nyerere amesema wabunge wanatakiwa kuijadili kwa kina ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu Akaunti ya
escrow kwa kuwa kuficha mambo kutaendelea kuzidisha matatizo nchini.
Alisema njia pekee ya kulimaliza suala hilo linalotarajiwa kuwasilishwa
bungeni leo, ni kwa wabunge kuijadili taarifa hiyo na kuchukua hatua
zinazostahili.
Mama Nyerere alisema hayo jana nyumbani kwake Msasani Dar es Salaam,
alipojibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua maoni yake
kuhusu escrow
kama suala hilo linatakiwa kujadiliwa au kutojadiliwa bungeni. “Jambo
hili sasa liko kwenye magazeti kwa muda mrefu, ningependa lijadiliwe na
wabunge limalizike kabisa, lisipojadiliwa tutatafuta matatizo makubwa
baadaye,” alisema.
Mama Nyerere alisema suala hilo linagusa masilahi ya umma, hasa katika
kipindi hiki ambacho wengi wanakosa huduma muhimu kutokana na uhaba wa
fedha unaoikabili Serikali.
“Wanaposikia ripoti za ukaguzi zinafichwafichwa wakati ndugu zao
wanakufa kwa kukosa dawa ni lazima watakuwa na hasira na baadaye
kusababisha machafuko,” alisema.
Hata hivyo, alisema katika Serikali ya Awamu ya Kwanza kulikuwa na wizi wa mali ya umma lakini hali iliyopo sasa ni ya kutisha.
“Wizi haujaanza leo, hata zamani watu walikuwa wanasogeza fedha za umma,
lakini sasa hivi hali imezidi kwenye vyombo vya habari kila siku ni
ufisadi, jambo muhimu ni kuchukua hatua haraka,” alisema.
Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment