Home » » WATALAAM WA TEHAMA WAPASWA KUTUMIA TEKNOLOJIA MPYA

WATALAAM WA TEHAMA WAPASWA KUTUMIA TEKNOLOJIA MPYA


Na Ally Daud-Maelezo
Wataalamu Wa tehama wamepaswa  kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ya tehama ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo  iliyopo kwa sasa ulimwenguni.
Hayo yamesemwa  leo jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Faustin Kamuzora  katika mkutano wa wadau wa tehama uliojadili utekelezaji wa mkakati wa Sera ya Tehama ya mwaka 2016
Aliongeza kuwa wataalamu wa tehama wanapaswa kutumia njia mpya na za kisasa ili kukuza uchumi kama zinavyofanya nchi zilizoendelea duniani.
"Wanatehama mnatakiwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ili kuweza kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati  kwa kupitia teknolojia hiyo kama zifanyavyo nchi nyingine zilizoendelea duniani kote" alisema Prof. Kamuzora.
Aidha Prof. Kamuzora alisema katika mkutano huo wanatarajia kupata mbinu mbadala za kupambana na uhalifu kwa kutumia mitandao katika kutekeleza mkakati wa Sera ya tehama ya mwaka 2016- 2020 ili kutekeleza mpango huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Clarence Ichwekeleza alisema kuwa moja ya mkakati wa mkutano huo ni kutengeneza miundombinu ya tehama kwa Watanzania waweze kufikiwa kirahisi.
Aidha mhandisi Ichwekeleza alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2018 inaandaa mkakati maalum wa kuwalinda watoto kutokana na madhara ya Tehama ili kuweza kuwasaidia watoto kukua katika misingi bora inayoendana na jamii ya Tanzania.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali Wa mitandao ya simu pamoja na wataalamu Wa tehama nchini  ili kujadili mkakati wa Sera ya Tehama ya mwaka 2016.
MWISHO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa