Home » » KUTOKA BUNDA: WENYEVITI WA VIJIJI NA MTAA MARUFUKU KUMILIKI MUHURI.

KUTOKA BUNDA: WENYEVITI WA VIJIJI NA MTAA MARUFUKU KUMILIKI MUHURI.

Katika kikao cha mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama cha mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bunda kilichofanyika siku ya tarehe 20/3/2025 katika ukumbi wa Malaika, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh. Aswege Enock Kaminyoge alisoma waraka wenye muongozo unaokataza wenyeviti wa vijiji na mitaa kumiliki muhuri.

Lengo la kusoma waraka huo ni baada ya wenyeviti wa vijiji na mitaa kuomba kumiliki muhuri hiyo kama kitendea kazi chao, kitu ambacho Mkuu wa Wilaya ilibidi kusoma waraka huo ambao umeelezea na kutolea ufafanuzi kwanini hawapaswi kuwa nao na vifaa ambavyo wanatakiwa kuwa navyo kama sehemu ya vitendea kazi.

Mh.Kaminyoge alisema wajibu wa mwenyekiti wa MTAA na Kijiji ni kusimamia, kuhamasisha, kufuatilia, kuongoza, kuwasilisha, kushirikisha, kusuluhisha, kuhifadhi na kudumisha amani katika MTAA au kijiji anachoongoza. 

Muongozo wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali mitaa wenye kumb. Na. CCB.126/215/01 wa tarehe 30/11/2016 unaelezea matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na vijiji kwamba wanatakiwa kuacha mara Moja kutumia mihuri katika majukumu ya kiutendaji na badala yake uwekaji au ugongaji wa mihuri ufanywe na maafisa watendaji wa eneo husika.

Pale ambapo MTAA au kijiji hakuna Mtendaji wa MTAA au kijiji, mwenyekiti wa MTAA au kijiji amtambulishe Mwananchi mwenye kuhitaji huduma ya kugongewa muhuri kwa Mtendaji wa kata ili aweze kugongewa muhuri wa kata.

Hivyo basi, kwa mujibu wa taratibu za kazi za mwenyekiti wa MTAA na Kijiji aliyechaguliwa na wananchi anatakiwa kuwa au kumiliki vifaa vifuatavyo ambavyo ni bendera yenye nembo ya Halmashauri, rejista ya wakazi wa MTAA au kijiji na daftari la mihtasari ya vikao vya MTAA au kijiji.

Mh. Kaminyoge aliwaagiza Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa maelekezo haya ili kuweza kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima katika mitaa na vijiji.

" Watendaji wa mitaa na vijiji watakaobainika kutumia mihuri vibaya na kuendeleza migogoro hususani ya ardhi watachukuliwa hatua Kali za kisheria." Alisema Mkuu wa Wilaya.





0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa