WAKATI
Mataifa mbalimbali yanaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani yanayofikia
kilele chake hapo Juni 5, 2017, takriban hekta 372,000 za misitu hupotea
kila mwaka nchini Tanzania kutokana na shughuli mbalimbali. Mwandishi
Beatrice Lyimo wa Idara ya Habari - MAELEZO anaelezea zaidi.
Kwa
miaka mingi siku ya Mazingira duniani imekuwa ikiadhimishwa kwa Wadau
katika nchi mbalimbali kuchukua hatua chanya zinazohusu mazingira. Siku
hii pia imekuwa ni sehemu ya kampeni ya utoaji elimu juu ya maswala
yanayojitokeza kuhusiana na mazingira.
Kauli
mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu inasema “Mahusiano Endelevu Kati
ya Binadamu na Mazingira” ikihamasisha jamii kuwa na urafiki endelevu na
mazingira asilia ambapo kila mtu anapaswa kutambua, kufurahi, kujivunia
na kulinda uzuri wa mazingira asilia na kuhamasishana ili kuyatunza na
kuyahifadhi.
Tanzania
kama ilivyo kwa nchi nyingi Barani Afrika na duniani kwa ujumla
imeendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira
unaotokana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, ujenzi
n.k
Mara
baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
aliagiza kutofanyika kwa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika ambayo
yalizoeleka na badala yake Watanzania waadhimishe siku hiyo kwa kufanya
usafi.
Mtazamo wa wengi kuhusiana na maelekezo ya Dkt. Magufuli ulilenga zaidi katika kubana matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Pamoja
na mtazamo huo Mhe. Rais aliona mbali zaidi, kwani usafi wa mazingira
unasaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, ambayo
yanaigharibu Serikali fedha nyingi zaidi ya zile ambazo zingetumika
katika kufanikisha maadhimisho hayo.
Hivyo
uamuzi alioutoa Mhe. Rais utakumbukwa zaidi wakati huu ambapo nchi
mbalimbali zinaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Siku hii inatutaka
tutoke nje tuone mazingira yetu yalivyo, tuone thamani yake na tupaze
sauti ya kuulinda ulimwengu tunamoishi.
Inakadiriwa takribani hekta 372,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na shughuli
za kilimo na ufugaji kwa njia zisizo endelevu. Uharibifu huu wa misitu
unachangia pia kukosekana kwa mvua, kukauka kwa mito, mabwawa na uoto wa
asili.
Akizungumza
katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwaka jana
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amesema kuwa
kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi
mazingira inahitaji ushirikiano wa Wadau katika ngazi zote.
Amesema,
Serikali inahitaji ushirkiano mkubwa kutoka kwa wananchi, Vyombo vya
Vabari, Taasisi na Asasi za Kiraia katika kutekeleza kikamilifu Sheria
na Kanuni za uhifadhi wa mazingira nchini ili kupunguza kwa kiasi
kikubwa uharibifu wa mazingira.
Aidha, Makamu
wa Rais alizitaka Mamlaka katika ngazi mbalimbali ziwe na Mipango bora
ya ardhi, mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, pamoja na udhibiti wa
uvunaji holela wa misitu na ufugaji usio endelevu.
Mama
Samia pia alizitaka Wizara na Taasisi zote za Serikali na zisizo za
Kiserikali kuendelea kutoa elimu juu umuhimu wa kutunza mazingira na
faida zinazopatikana ili Wananchi waunge mkono jitihada zinazofanywa
katika kulinda na kuhifandhi mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na
kijacho.
“Usafi
wa mazingira uhusishe kila mtu kuhakikisha taka zinakusanywa na
zinatupwa katika maeneo yaliyotengwa na tupande miti mingi wakati wa
msimu wa mvua ili tujihami na kuenea kwa hali ya jangwa na mabadiliko ya
tabianchi” alisema Mhe. Samia.
Akiwasilisha
hotuba ya makadirio ya hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa
mwaka 2017/18, Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira), January Makamba
amesema kuwa uchumi wa Tanzania unategemea kwa kiasi kikubwa maliasili zilizopo ikiwemo ardhi, maji, misitu na hewa safi.
Alisema, maliasili zilizopo zinahitajika kwa matumizi ya vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo uwepo wake hutegemea zaidi uhifadhi wa rasilimali hizo na matumizi katika jamii inayotuzunguka.
Aidha, Waziri Makamba alibainisha baadhi ya Changamoto iliyopo kwa sasa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu uhifadhi ya mazingira na uwepo wa mabadiliko ya tabianchi. Hivyo juhudi kubwa inahitajika zaidi katika kutoa elimu kuhusiana na mazingira.
Kwa
mujibu wa Waziri Makamba, Serikali imeanisha programu mbalimbali za
uhifadhi mazingira kwa kutengeneza, kusimamia na kuhamasisha utekelezaji
wa mipango na mikakati ya Kitaifa ya hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini katika ngazi mbalimbali za utawala.
“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali iliwahimiza viongozi na watendaji katika Sektretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta zote Tanzania Bara kutenga fedha na kutekeleza na kutolea taarifa mikakati na mipango ya hifadhi na usimamizi wa mazingira” alisema Mhe. Makamba.
Aliongeza
kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na
Utalii na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliandaa Mkakati wa Taifa wa Kupanda na Kutunza Miti utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2016 hadi 2021) ambapo mkakati huo unaelekeza katika kila kijiji, kitongoji, mtaa na kaya .
Amesema, Mkakati huo umezingatia kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika mikakati
na kampeni zilizopita, ikiwemo motisha na ushiriki wa sekta binafsi
katika biashara ya misitu ambapo baadhi ya mikoa imeanza utekelezaji wa
mkakati huo kwa kupanda miti kwenye maeneo yao.
Tarehe
5 Juni kila mwaka Tanzania tunaungana na mataifa mengine duniani
kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, ambapo kampeni mbalimbali
huandaliwa kwa ajili ya kuhamasisha jamii kujenga uelewa wa masuala yahusuyo mazingira kuchukua hatua stahiki za kuhifadhi na kulinda mazingira.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment