Home » » Ndoa ya mwanafunzi yamtesa mwalimu

Ndoa ya mwanafunzi yamtesa mwalimu

 na Christopher Nyenyembe, Musoma
MWALIMU wa Sekondari ya Mkono wilaya ya Musoma Vijijini, Shigita Katisho, amelalamikia kitendo cha kutishwa na kufanyiwa vitendo vya kishirikina baada ya kumripoti mwalimu mwenzake (jina tunalo), aliyekuwa akifanya mapenzi na mwanafunzi, kisha akaamua kumuoa na kuishi naye kwenye nyumba za shule.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa mwalimu huyo amelalamikia kitendo cha ofisa elimu wa wilaya hiyo kushindwa kumhamisha baada ya tukio hilo linaloonekana kuhatarisha maisha yake.
Katisho alisema kuwa baada ya kugundua kuwa mwalimu mwenzake anafanya ngono na mwanafunzi wa kidato cha nne (jina tunalo), aliamua kutoa taarifa kwa ofisa elimu ili achukuliwe hatua lakini kinyume chake amejikuta akinyanyaswa yeye kwa kusimamishiwa mshahara wake.
Mwalimu Katisho mwenye namba ED/PF 59509, alidai kuwa baada ya kuripoti tukio hilo amekuwa akipokea vitisho na kufanyiwa vitendo vya kishirikina vinavyotishia usalama wake.
Hata mshahara umeondolewa kwenye akaunti yake ya Benki ya NMB Wilaya ya Kahama na kuhamishiwa kwenye akaunti ya mwalimu mwingine wa Shule ya Sekondari Isagehe.
Ofisa Elimu Taaluma wilaya ya Musoma Vijijini, Saverine Mishinde, alipohojiwa kwa njia ya simu, alikiri kutokea kwa tukio la mwalimu huyo kutoa taarifa zinazomhusu mwalimu mwenzake aliyekuwa na mahusiano ya mapenzi na mwanafunzi wa shule hiyo.
“Ni kweli tulipokea taarifa hizo lakini kinachomtesa mwalimu Katisho ni utoro, amekuwa akitoroka kituo chake cha kazi na sioni kama sababu anayoiogopa ni ile ya kutoa taarifa, alikuwa wilaya ya Kahama na huko ndiko wakamhamishia mshahara wake sisi hatuhusiki,” alisema.
Chanzo Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa