na Ahmed Makongo, Bunda
KANISA la Anglikana Dayosisi ya Mara, limechimba zaidi ya visima virefu 15, katika wilaya za Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji wakazi wa maeneo hayo.
Askofu wa kanisa hilo, Hilkiah Omindo, alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kisima kirefu cha maji kilichochimbwa na kanisa hilo katika kijiji cha Karukekere, wilayani hapa.
Alisema wamechimba visima hivyo ambavyo kila kimoja kimegharimu zaidi ya sh milioni 4.8 katika vijiji vya wilaya za Musoma Vijijini, Tarime, Rorya, Bunda na Serengeti, lengo likiwa kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji wakazi wake.
Askofu Omindo alisema kuwa zoezi hilo la uchimbaji visima sambamba na utoaji huduma nyingine za kijamii kupitia kitengo cha kanisa hilo cha huduma za kijamii ni endelevu.
“Zoezi hili la kuchimba visima ni endelevu, ikiwa ni pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya kijamii, pindi tunapopata uwezo wa kufanya hivyo...tunaamini kisima hiki kitawasaidia kupata huduma ya maji wakazi wa kijiji hiki,” alisema.
Akizindua kisima hicho Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, alilishukuru kanisa hilo kwa misaada ya kijamii wanayoendelea kuitoa wilayani hapa, na kwamba serikali inatambua mchango huo, ambao lengo lake ni kuondolea kero wananchi na kuwaletea maendeleo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment