Home » » WALIMU MARA WATANGAZA KUSHIRIKI MGOMO

WALIMU MARA WATANGAZA KUSHIRIKI MGOMO


Walimu wilayani Bunda, mkoani Mara, wamesema wako tayari kushiriki kwenye mgomo utakaotangazwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iwapo serikali haiwezi kutekeleza madai  yao ikiwemo kupandishiwa mishahara kwa asilimia 100.



Tamko hilo wamelitoa juzi kwa nyakati tofauti, kwenye mikutano iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kabaribu, mikutano iliyoitishwa na chama cha walimu (CWT) wilayani hapa.

Walimu hao walisema wako tayari kushiriki kwenye mgomo utakaotangazwa na baraza la chama cha walimu taifa, wakidai ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia masomo ya Sayansi asilimia 55, sanaa asilimia 50, pamoja na asilimia 30 ya walimu wanaofundisha katika mazingira magumu.

Walisisitiza kwamba iwapo serikali itashindwa kuwajali walimu na kuwaondolea kero mbalimbali zinazowakabili, kiwango cha elimu kwa shule zao hakiwezi kupanda, kwani hawawezi kufanya kazi huku hawapati maslahi mazuri.

Awali, Mwenyekiti wa chama cha walimu wilayani hapa, Ruhumbika Furancis,  ameomba walimu wote wilayani hapa washiriki kikamilifu, kwani utafuata taratibu zote za kisheria.

Mikutano hiyo iliyohudhuriwa na Mwenyekiti wa CWT mkoani Mara, Livingstone Gamba, ambaye alisema sasa hivi walimu wameingia katika mgogoro mkubwa na Serikali mpaka hapo itakapowatekelezea  madai yao.

Kikao hicho kilishirikisha walimu wote wa shule za msingi na sekondari za wilayani ya Bunda.




CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa