na Berensi Alikadi, Bunda
SERIKALI wilayani Bunda, mkoani Mara, imewaonya watendaji wa serikali katika ngazi za vijiji na kata wanaojihusisha na kuhujumu vocha za pembejeo kwa wakulima kuacha mara moja la sivyo watachukuliwa hatua kali.
Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Mirumbe, wakati akihutubia wananchi wa vijiji vya Tarafa ya Nansimo ikiwa ni sehemu yake ya kujitambulisha tangu ateuliwe na rais kushika wadhifa huo.
Alisema kuwa lipo tatizo hilo la watendaji wa ngazi za vijiji kata na hata wataalamu ugani kuhujumu vocha za wakulima na kujipatia fedha huku wakijua fika kufanya hivyo ni kosa la jinai na kwamba kuanzia sasa kiama chao kimefika.
Mirumbe aliwatahadharisha kuwa mbinu zao anazozifahamu kwa vile naye alikuwa mtumishi katika wilaya hiyo kwa hiyo atakeyegundulika atachukuliwa hatua za kisheria pasipo kumuonea aibu.
‘‘Bado tunaendelea na mchakato tukikubaini sheria itachukuwa mkondo wake, hivyo ndugu zangu nawatahadharisha sana naomba muniangalie kwa macho mawili kwa hili tutaonana wabaya,’’ alisema.
Aliwataka wataalamu walioko katika halmashauri hiyo kutumia utaalamu wao ili kuhakikisha wanaleta mabadiliko katika halmashauri hiyo na wilaya kwa ujumla kwani ni muda mrefu sasa wilaya hiyo imekuwa ikitajwa kuwa ya mwisho kwa umaskini nchini licha ya kuwa na rasilimali nyingi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment