Home » » Mkandarasi alalamikiwa

Mkandarasi alalamikiwa


na Mwandishi wetu, Bunda
BAADHI ya wakazi wa mji wa Bunda na vijiji vitatu katika halmashauri ya wilaya hiyo, wameiomba serikali kusitisha mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Nyakirang’ani Construction Ltd, iliyopewa kazi ya kuchimba mtaro wa kutoa maji Ziwa Vctoria kupitia  vijiji hivyo hadi mjini Bunda.
Mradi huo mkubwa wa maji unaotekelezwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na serikali unakusudia kugharimu sh bilioni 30 huku kampuni hiyo ikipewa kazi ya kuchimba mtaro na kuweka mabomba kwa gharama ya zaidi ya sh bilioni 6.7.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wakazi hao wa vijiji hivyo vya Guta, Tairo, Nyantareja na mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, walisema kasi ndogo ya uchimbaji mtaro huo inachangia kutokamilika kwa wakati kwa mradi unaotegemewa na wakazi zaidi ya laki moja katika maeneo hayo.
“Wakati Waziri Stephen Wassira amekuja kukagua shughuli za uchimbaji wa mtaro, mkandarasi alionekana kwenda kasi lakini alipoondoka tu, alihamisha vifaa,” alisema Nyanjura Magafu mkazi wa Kijiji cha Tairo.
Naye mwananchi mwingine wa mjini Bunda, Emmanuel Sagati, alisema kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa mtaro huo kunakwamisha kuanza kwa hatua ya pili ya kusambaza maji kwa wananchi, huku akiitaka serikali kuona namna ya kutafuta mkandarasi mwingine mwenye kufanya kazi kwa wakati.
Mmoja wa maafisa katika Idara ya Maji mjini Bunda, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema wakati Waziri Wassira ambaye pia ni mbunge wa Bunda, akikagua mradi huo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ujenzi, Mahuza Mmangi, alimweleza kuwa mtaro huo ungekamilika ndani ya wiki nne lakini hadi sasa hakuna dalili hizo.
“Ndugu yangu sisi wengine hapa ni wadogo hatuwezi kulizungumzia hili suala kwa undani, nadhani huyu jamaa ana watu wanamlinda huko juu ndiyo maana anachelewesha kazi hii la sivyo huu umekuwa mtaji wa CCM wa kuombea kura kwa kila uchaguzi,” alisema ofisa huyo.
Alipoulizwa kuhusu kusuasua kwa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Cyprian Oyier, alikiri mradi huo kutekelezwa kwa kasi ndogo na kwamba huenda mkandarasi ameelemewa na kazi katika maeneo mengine.
“Hata mimi nashangaa kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huu kwani sasa hata mitambo imeondolewa eneo la mradi sijui huyu mkandarasi amezidiwa na kazi sehemu nyingine,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa