Na Shomari Binda,Musoma.. Mara yetu Blog
JAMII Mkoani Mara imetakiwa kutoa maoni katika tume ya mchakato wa kupata katiba mpya yatakayoelezea ukuaji wa uhusiano wa jinsia katika jamii ili kuingizwa kipengele cha adhabu kali katika masuala ya ukatili wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa Mjini Musoma na Mwenyekiti wa asasi za kirai katika Manispaa ya Musoma, Jenipher Danga katika mdahalo uliokuwa ukielezea ukuaji wa uhusiano wa kijinsia katika mchakato wa kupata Katiba mpya iliyoratibiwa na asasi ya Mara Forum Development kwa kushirikiana na asasi za kiraia.
Danga alisema kuwa fursa iliyopo kwa Watanzania katika mchakato wa kupata Katiba mpya inabidi waifanyie kazi katika kutoa maoni yao ili katiba ijayo iwe suluhisho ya kero mbalimbali zinazo jitokeza katika jamii.
“Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani katika Mkoa wa Mara jammii itoe maoni ya ukatili huo na adhabu zake katika tume ya kukusanya maoni ya mchakato wa kupata Katiba mpya ili kipengele na kifungu cha adhabu kali kiweze kuwekwa” alisema Danga
Alisema kuwa suala la usawa na haki katika jamii linalokemea na kufuta mfumo dume litakuwa na nguvu iwapo liwekwa kwenya katiba na hivyo kupunguza ama kutokomeza kabisa tatizo hilo.
Kwa upande wake mratibu wa asasi ya Mara Development Forum, Gerorge Chibasa alisema lengo la kuandaa midahalo hiyo ni kuijengea jamii uwezo wa ufahamu zaidi kabla tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya haijafika Mkoani Mara ili pindi tume hiyo itakapofika mkoani humo waweze kuchangia maoni yao kikamilifu.
Alisema katika midahalo hiyo ambayo inafanyika katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara mada mbalimbali zimekuwa zikitolewa na wataalamu mbalimbali na kwamba mwitikio wa jamii umekuwa ni mkubwa.
Midahalo hiyo inafanyika kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation For Civil Society ambao ndio wamewezesha kuwafikia Wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara na kuelezea umuhimu juu ya mchakato wa kupata Katiba mpya. |
0 comments:
Post a Comment