na Mwandishi wetu, Tarime
PIKIPIKI iliyotolewa msaada na Pact Tanzania imezua mgogoro kati ya Mkurugenzi wa Halmashauri na Ofisa Ustawi wa Jamii huku kila mmoja akidai pikipiki hiyo imetolewa kwa ajili ya ofisi yake.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Tarime, Piter Mwanga, alisema pikipiki zilizotolewa kwa ufadhili wa Pact Tanzania zilitolewa kwa kila ofisa ustawi wa jamii katika wilaya zote mkoani Mara kupitia kwa wakurugenzi wa halmashauri.
Mwanga alisema baada ya kutolewa kwa pikipiki hizo, yeye ndiye hajapata kwa madai kuwa baada ya pikipiki hiyo kutumwa kwake kupitia kwa Mkurugenzi wa Halamashauri ya Tarime, Fidelis Lumato, alikataa kumkabidhi na badala yake imekabidhiwa katika Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya.
“Pikipiki zilitolewa kwa kila ofisa ustawi wa jamii wilaya. Kila mtu pikipiki moja kwa ajili ya kuendeshea shughuli mbalimbali, wenzangu wote wilayani walishapata isipokuwa mimi,” alisema Mwanga.
Mwanga alisema mbali na kudhulumiwa pikipiki, kitengo hicho cha ustawi wa jamii kimekuwa kikipuuzwa na hata kutoshirikishwa katika semina mbalimbali za ustawi wa jamii na vikao mbalimbali na kwamba watu wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakiingilia na kufanya shughuli za ustawi wa jamii huku walengwa wakiachwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Fidelis Lumato, alisema pikipiki hiyo ilitolewa na Pact Tanzania kuja Ofisi ya Mkurugenzi ambapo yeye aliitoa kwenda katika idara yake ya maendeleo ya jamii.
“Mimi sing’ang’anii pikipiki, tuna pikipiki nyingi. Hii imetumwa kuja ofisi ya mkurugenzi kupitia maelekezo ya Pact ambapo barua ilitumwa ofisini kwangu. Kama ilitolewa kwenda ustawi wa jamii ingetumwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa sababu kitengo hicho cha jamii kipo chini ya ofisi hiyo,” alisema Limato.
Mkurugenzi huyo alimtaka Ofisa Ustawi huyo kuwasiliana na wafadhili hao kujua ukweli na nani anayepaswa kupata pikipiki na kwamba Pact kama watasema ni ya Ustawi wa Jamii wilaya, atawakabidhi pikipiki hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment