na Sitta Tumma, Tarime
BARAZA la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limemtaja mbunge wa zamani wa jimbo hilo, marehemu Chacha Wangwe (CHADEMA), kuwa ni kiongozi shupavu aliyebadilisha maisha ya wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwaletea neema ya kimaendeleo, kuliko ilivyo sasa katika uongozi wa CCM jimboni hapa.
Kulingana na hayo, BAVICHA imewasihi wananchi wa Tarime kuunganisha nguvu zao pamoja na viongozi wa CHADEMA katika vuguvugu la kutaka kuleta mabadiliko ya kiutawala hapa nchini, ikiwa ni kuhakikisha wanaiondoa CCM madarakani wakati wa uchaguzi mkuu 2015.
Mwenyekiti wa BAVICHA taifa, John Heche aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika Komaswa wilayani hapa, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaomba wana Tarime na Watanzania wote kwa ujumla kutowachagua watu wanaotoa rushwa ya fedha, khanga, kofia na chumvi wakati wa uchaguzi.
Alisema, wakati umefika sasa wananchi kukataa kurubuniwa na CCM kwa kupewa vitu vidogo ili viongozi wake wawachague, kiongozi anayetoa rushwa na baadaye wananchi wakamchagua kamwe hatawaletea maendeleo ya kisekta, badala yake kiongozi huyo atabaki kujineemesha yeye binafsi.
”Katika nchi hii, na hata sisi hapa Tarime tunatambua kabisa kwamba marehemu Chacha Wangwe alikuwa kiongozi shupavu aliyebadili maisha ya wananchi wake.
”Kwa hiyo lazima tutafakari na kufanya maamuzi ya kweli katika kuleta mabadiliko ya maendeleo kwa kuichagua CHADEMA 2015. Tuunganisheni nguvu pamoja ili tuiondoe CCM madarakani mwaka wa uchaguzi mkuu,” alisema Heche katika mkutano huo.
Pia mwenyekiti huyo wa BAVICHA taifa aliwaambia wananchi hao kwamba, serikali ya CCM inaonekana imefikia ukomo wa kuwaletea maendeleo wananchi, licha ya kuwa na rasilimali nyingi ambazo baadhi yake hazipatikani kote duniani isipokuwa Tanzania tu.
Kwa mujibu wa Heche Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa kuwa ombaomba misaada nje ya nchi, ikiongozwa na Iraq pamoja na Afghanistan zilizoathiriwa uchumi wake na migogoro ya kivita miaka mingi, hivyo Watanzania ni vema wakafanya maamuzi magumu ya kuiangusha CCM kupitia visanduku vya kura mwaka huo wa uchaguzi mkuu.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA wilayani Tarime (Bawacha), Mary Nyagabona, Katibu wa Bawacha, Veronica Machohe na mjumbe wa kamati tendaji CHADEMA wilayani hapa, Ghati Nyerere, waliwaomba wanawake kukataa kurubuniwa na CCM wakati wa uchaguzi.
”Ninyi wanawake ndio mnaotuangusha, mnarubuniwa wakati wa uchaguzi kwa kupewa chumvi na vilemba. Acheni kutumiwa maana huko ni kujirudisha nyuma....njooni CHADEMA tuunganishe nguvu tupiganie maendeleo yetu sote,” alisema Nyagabona.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment