Home » » HECHE AZUA GUMZO

HECHE AZUA GUMZO


na Ambrose Wantaigwa, Tarime
UAMUZI wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) wa kutangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Tarime 2015 umepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wilayani hapa.
Baadhi ya wananchi waliunga mkono hatua hiyo, wengine wakidai kuwa sio wakati muafaka wa kutangaza uamuzi huo, kwa kuwa unaweza kukigawa chama chake.
Muniko Chacha aliyejitambulisha kuwa ni mwanachama wa CHADEMA, alisema kwa kuwa Heche amekabidhiwa madaraka makubwa katika chama, angetumia muda mwingi kuwatumikia wakazi jimboni humo badala ya kufikiria ubunge.
“Nakubaliana kuwa ni demokrasia kwa mtu yeyote kushiriki katika siasa ikiwa ni pamoja na haki ya katiba ya nchi kugombea nafasi yoyote ya uongozi, lakini kila jambo lina wakati muafaka wa kufanya hivyo si kila wakati kuzungumzia masuala ya kisiasa,’’ alisema.
Alibainisha kuwa hatua hiyo inaweza kuleta mgawanyiko mkubwa katika chama ngazi ya wilaya iwapo wanachama wengine wanaohitaji nafasi hiyo wataanza kuchukua uamuzi huo kwa sasa.
Kwa upande wake, Julius Makima, mkazi wa Sirari, alimuunga mkono Heche kwa kusema ana uwezo wa kutetea masilahi ya jimbo hilo kwa kuwa hilo lilithibitika alipokuwa diwani wa Kata ya Tarime.
Alisema Heche ameonesha ukomavu wa kisiasa katika jitihada zake za kuunganisha koo zote za kabila la Wakurya na kuepusha mapigano ya mara kwa mara.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Sokoni katika mji mdogo wa Sirari mapema wiki hii, Heche aliweka bayana msimamo wake huo wa kugombea ubunge wa Jimbo la Tarime katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015 kupitia CHADEMA.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa