Home » » BAVICHA YAIBUA ‘MADUDU’ TARIME

BAVICHA YAIBUA ‘MADUDU’ TARIME


na Sitta Tumma, Tarime
BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo –Taifa (BAVICHA), limefichua 'madudu' ya Ofisa Mtendaji mmoja wa wilayani Tarime anayedaiwa kuhamishia vifaa na shughuli za ofisi nyumbani kwake, kinyume na taratibu na sheria za nchi.
Tayari baraza hilo limemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kumchukulia hatua kali za kinidhamu.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa ‘Vuguvugu la Mabadiliko’ (M4C), uliofanyika wilayani hapa.
Alisema, Mkurugenzi huyo wa halmashauri anapaswa kumwajibisha mtendaji huyo ikiwa ni pamoja na kumwamuru kurejesha vifaa vya serikali katika ofisi yake ya Kata, vinginevyo atakwenda kumshtaki kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusiana na kufumbia macho vitendo hivyo.
Alisema, kitendo cha mtendaji huyo kamwe hakivumiliki na kwamba lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya mhusika.
"Nimeambiwa hapa na wananchi kwamba mtendaji wa kata hii kahamishia ofisi nyumbani kwake. Nasema kitendo hiki ni kibaya na hakivumiliki hata kidogo. Kwa hiyo namwamuru mtendaji huyu arudishe vifaa na shughuli za kiserikali ofisini kwake.
"Pia, nitaenda kuzungumza na Mkurugenzi ahakikishe ndani ya muda mfupi awe amemchukulia hatua kali mtendaji wake huyu. CHADEMA hatuwezi kufumbia macho udhalimu wa namna hii,” alisema.
Awali, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Tarime, Mwita Marwa Mroni, Mwenyekiti wa BAVICHA wilayani hapa, Chacha Heche, Mjumbe wa kamati tendaji, Ghati Nyerere na Katibu wa Baraza la Wanawake wilayani Tarime, Veronika Machohe waliwaomba wananchi wa Muriba na wilaya hiyo kwa ujumla, wakatae kutumiwa na CCM kama daraja wakati wa uchaguzi.
"Enyi vijana wenzangu, baba zangu na mama zangu CCM imekosa dira wala mwelekeo wa kuwaletea maendeleo. Leo hii tunaishi kwa shida na tabu tupu kwa sababu ya CCM imeshindwa kutusaidia. Tunawaombeni sana tuunganisheni nguvu pamoja na CHADEMA tuing'oe CCM madarakani mwaka 2015", alisema Chacha Heche.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa