na Ahmed Makongo, Bunda
KATIKA kutekeleza sera ya serikali ya kila kijiji kuwa na zahanati, ili wananchi waweze kupata huduma ya afya kwa ukaribu zaidi, wananchi wa vijiji viwili vya Nyatwali, pamoja na Kabasa wilayani Bunda, katika Mkoa wa Mara, wameanza kutekeleza sera hiyo.
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Rainer Kapinga, alisema kuwa katika Kijiji cha Kabasa wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, pamoja na serikali kuu wamefanikiwa kujenga zahanati kijijini hapo.
Dk. Kapinga alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo umeanza Machi mwaka 2010 na unajumuisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lililogharimu kiasi cha sh milioni 115 na jengo la huduma za afya ya uzazi na mtoto (RCH), lililogharimu kiasi cha sh milioni 88.
Alisema kuwa ujenzi wote umegharimu jumla ya sh 208,500,000, ambapo serikali kuu imechangia kiasi cha shilingi milioni 203, nguvu za wananchi sh milioni mbili na mchango wa halmashauri ya wilaya sh milioni 3.5.
Alifafanua kuwa kwa sasa zahanati hiyo inahudumia vijiji vitatu vya Kabasa, Kung’ombe na Nyasana, vyenye jumla ya wakazi 8,184.
Aidha, Dk. Kapinga alisema kuwa pia kijiji cha Nyatwali katika Kata ya Kunzugu, kimefanikiwa kujenga zahanati moja kwa ufadhili wa Nyanza Road Works Company Limited ya mkoani Mwanza, ambaye ni mwekezaji wa ndani ya kijijini hapo.
Dk. Kapinga alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi Januari mwaka huu, na utakamilika mwezi Septemba mwaka huu na kwamba itakapokamilika itahudumia jumla ya wakazi 7,895 wa vijiji viwili vya Nyatwali na Serengeti.
Alisema kuwa hadi kukamilika kwake itagharimu kiasi cha sh milioni 262, ambapo Nyanza Road Works Company Limited imetoa sh milioni 260 na wananchi wametoa eneo la ardhi lenye ukubwa wa eka tatu, lenye thamani ya sh milioni mbili.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment