na Berensi Alikadi, Bunda
WENYEVITI wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bunda, mkoani Mara wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kutimiza ahadi yake ya kuipatia Hospitali ya Manyamanyama vifaa mbalimbali likiwemo gari la wagonjwa, ili iweze kupandishwa hadhi na kuwa ya wilaya.
Wakichangia katika kikao cha baraza la mji mdogo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Pastory Ncheye, wenyeviti hao walisema rais aliahidi kuipatia hospitali hiyo vifaa mbalimbali alipofanya ziara mwaka 2006, lakini hadi sasa hajatimiza ahadi hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Manyamanyama, Mgendi Makanayanga, alisema wananchi wanapata shida ya matibabu kutokana na hosptali teule ya DDH inayomilikiwa na Kanisa la Kilutheri kushindwa kutoa huduma ipasavyo.
Alisema hospitali hiyo licha ya kushindwa kutoa huduma, pia mazingira yake kwa sasa ni machafu.
Aidha, alisema vyoo yake vimejaaa na wagonjwa wanaokwenda kujifungua hulazimishwa kufanya, usafi kitu ambacho ni kinyume na sheria za kazi.
‘’Ndugu zangu nataka niwaambie tutasumbua vichwa sana kwa vile tunayo hospitali yetu ya Manyamanyama na kwa vile rais aliahidi kutusaidia vifaa, tumuombe sasa atimize ahadi yake, ili iweze kuwa ya wilaya,” alisema.
Naye Ofisa Mtendaji wa mamlaka hiyo, Charles Machage, alisema tatizo la Hospitali ya DDH limeshakuwa sugu kwani licha ya kubadilisha waganga, bado huduma zake si za kuridhisha, hivyo akaungana na wenyeviti hao kutaka Hospitali ya Manyamanyama iwe ya wilaya.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment