Home » » OPERESHENI VUA GAMBA VAA GWANDA YAZOA TARIME

OPERESHENI VUA GAMBA VAA GWANDA YAZOA TARIME


na Sitta Tumma, Tarime
OPERESHENI maalumu ya 'Vua gamba vaa Gwanda' inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imeitikisa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, baada ya zaidi ya wanachama 3,500 wakiwemo viongozi wa CCM kujiunga na CHADEMA.
Wanachama hao wakiwemo viongozi wa CCM, wamejiunga rasmi na CHADEMA mwishoni mwa wiki, wakati wa mkutano wa hadhara wa chama hicho, uliofanyika mjini Sirari kisha kuhutubiwa na mwenyekiti wa Baraza la Vijana taifa wa chama hicho (BAVICHA), John Heche.
Miongoni mwa viongozi wa CCM waliorudisha kadi kisha kukabidhiwa za CHADEMA mkutanoni hapo, ni pamoja na mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Sirari, Masha Vincent na mkewe Veronika Masha.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wengine wapya waliojiunga na chama hicho kikuu cha upinzani nchini mara baada ya kukabidhiwa kadi, Masha alisema wamechukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na kile alichodai majungu, fitina na uhasama unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wilayani hapa.
Alisema, enzi za CCM zinaonekana kuelekea kuisha, hivyo kujiunga kwao na CHADEMA ni kuongeza vuguvugu la mabadiliko, na kuwaomba vijana kufanya maamuzi ya dhati katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini.
Awali, mwenyekiti wa BAVICHA taifa, Heche aliwaomba Watanzania kutumia kura zao vizuri uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 pamoja na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika nchini mwaka 2015 kwa kuipigia kura CHADEMA ili ishike dola na kuleta mabadiliko ya kweli katika maendeleo ya wananchi.
Alisema, CHADEMA imedhamiria kuleta ukombozi mpya kwa wananchi wa taifa hili, na kwamba iwapo itawezeshwa kuingia madarakani mwaka 2015, itahakikisha serikali yake inatumia vizuri rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania wenyewe na si wawekezaji.
Aidha, akiwa katika mkutano wa hadhara Muriba Tarime, Heche alilaani vikali mauaji ya vijana yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya askari polisi katika mgodi wa dhahabu wa Nyamongo uliopo wilayani hapa, na kusema upo uwezekano wa kuishtaki serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC).
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa