Mwandishi wetu, Bunda-Mara Yetu
WATU wawili akiwemo mwanafunzi mmoja wa sekondari, wamekufa maji na wengine watatu wamenusurika baada ya mtumbwi wao kuzama wakati wakivua samaki katika ziwa Victoria, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Habari zinaeleza kuwa tukio hilo tukio hilo limetokea juzi majira saa 9:00 alasiri katika kijiji cha Mwitende, tarafa ya Nansimo wilayani Bunda, mkoani Mara.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mwitende Athanas Rwoga, amewataja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni David Fabian Daud, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Nansimo, iliyoko wilayani hapa na kwamba mwingine aliyekufa maji ni Ndebire Abdallah, mkazi wa kijiji hicho.
Habari kutoka kijijini hapo zinasema kuwa watu hao walikuwa wakivua samaki kwa kutumia kokolo, na kwamba ghafula mtumbwi wao ulijaa maji na kuzama umbali wa mita mia moja kutoka nchi kavu.
Imeelezwa kuwa ndani ya mtumbwi huo kulikuwa na watu watano, ambapo watatu kati yao waliokolewa na wananchi baada ya kupiga kelele za kuomba msaada.
Aidha, imeelezwa kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana siku hiyo saa 1:00 jioni, ambapo sasa wananchi bado wanaendelea na juhudi za kutafuta mwili wa mvuvi mwingine.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment