Home » » MKONO KUMJENGEA NYUMBA MWALIMU WA SAYANSI

MKONO KUMJENGEA NYUMBA MWALIMU WA SAYANSI

Na Mwandishi Wetu, Butiama
MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, ametangaza kumjengea nyumba ya kisasa kila mwalimu wa somo la sayansi atakayekubali kufundisha somo hilo wilayani Butiama.

Akizungumza na ujumbe wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Butiama, kabla ya chama hicho kumkabidhi hati maalumu ya kutambua mchango wake katika sekta ya elimu, alisema pamoja na kumjengea nyumba kila mwalimu wa somo hilo, pia atatoa fedha kwa ajili ya Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) kwa kila shule yenye mchepuo wa masomo ya sayansi kuanzia sasa.

Alisema lengo la hatua hiyo ni kuvutia walimu zaidi kufanya kazi katika eneo la Butiama, hasa kwa walimu wa sayansi ambao ni wachache katika shule za sekondari.

Aliuambia ujembe huo kuwa kulingana na mabadiliko makubwa ya dunia ya sayansi na teknolojia, hakuna budi sasa kuongeza kasi katika ufundishaji wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za dunia.

“Natangaza kuwa mwalimu yeyote wa somo la sayansi atakayekubali kuja kufundisha katika Wilaya ya Butiama aje nimjengee nyumba nzuri na ya kisasa aweze kufanya kazi yake bila kupata tatizo la makazi,” alisema Mkono na kuongeza:

“Mbali na nyumba, pia nitatoa fedha za kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa kwa kila shule ya mchepuo wa sayansi katika wilaya yangu, lengo langu likiwa ni kuwavutia walimu zaidi kuja katika eneo hili na kufundisha bila vikwazo vyovyote.”

Kuhusu migomo ya walimu iliyojitokeza, alishauri chama hicho kuanzia sasa kabla ya kufikia hatua hiyo kukutana nao kuona jinsi ya kutatua matatizo yao badala ya kugoma na kuwapa mateso wanafunzi.

“Najua walimu wamekuwa na matatizo makubwa na kila leo mmekuwa na migomo, sasa ushauri wangu hapa kwangu kabla hamjafikia hatua hiyo mnishirikishe tuone njia sahihi ya kutatua matatizo yenu, kabla ya kuwapa mateso wanafunzi wetu,” alisema Mkono.

Akitoa salamu kabla ya kukabidhi hati hiyo, Katibu wa CWT Wilaya ya Butiama, Wanjara Nyeoja, alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na mbunge huyo katika sekta ya elimu, hasa kwa kujenga shule nzuri na za kisasa, zikiwamo nyumba za walimu katika jimbo hilo.

Aidha, alisema bado sekta ya elimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki zinazowakabili shule za msingi na sekondari likiwamo tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za walimu.

“Walimu hususani maeneo mengi ya vijijini wanafundisha katika mazingira magumu kwa kukosa nyumba za kuishi hata kufikia walimu wengi kufikia hatua za kuhama wilaya yetu na kusababisha upungufu mkubwa wa walimu na wanaobaki sasa wanazidiwa kazi ya kufundisha watoto wetu,” alisema Nyeoja.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa