Home » » RCC YAIGAWA WILAYA YA BUTIAMA

RCC YAIGAWA WILAYA YA BUTIAMA

Mwandishi wetu, Mara Yetu
KIKAO cha kamati ya ushauri  ya mkoa wa Mara (RCC) kimepitisha mapendekezo ya kuigawa wilaya mpya ya Butiama kuwa na halmashauri mbili ambazo zitakuwa ni  halmashauri ya Butiama na Musoma vijijini ambapo kila moja itakuwa na jumla ya kata 17 .

Mapendekezo hayo yalipitishwa na wajumbe wa kikao hicho maalumu cha kamati ya ushauri ya mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa  wa Mara katika wilaya ya Musoma.

Katika kikao hicho wajumbe walipitisha maazimio hayo ambayo yalikwisha pitishwa katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ya Butiama (DCC) ambapo kikao hicho pia kiklitengua maamuzi ya makao makuu ya Musoma Vijijini yaliyokuwa yamependekezwa na DCC.

Wajumbe wa kamati hiyo ya ushauri ya mkoa walitengua makao makuu ya halmashauri ya Musoma kuwa Suguti na badala yake walipendekeza makao makuu yawe katika kijiji cha Murangi kwa madai kuwa eneo hilo ndilo eneo lililo katikati ya vijiji vyote  na kwamba eneo hilo ndilo eneo ambalo serikali imewekeza majengo mengi  na pia huduma za kijamii kama vile zahanati na maji.

Katika kikao hicho pia waliakubaliana kuwa wakazi wa halmashauri ya Musoma wanaweza kuhudumiwa na mkuu wa wilaya ya Musoma kwa kile walichodai kuwa halmashauri hiyo ipo jirani zaidi na ofisi ya Musoma Manispaa kuliko ofisi ya mkuu wa wilaya ya Butiama.

Hata hivyo Mwenyekiti wa kikao hicho Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Jackson Msome ambae ni mkuu wa wilaya ya Musoma alisema kuwa wakazi hao watahudumiwa popote kati ya Butiama au Musoma wakati wakisubiri mapendekezo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa