Home » » FAMILIA YA DIWANI ALIYEUAWA YAWAVAA POLISI

FAMILIA YA DIWANI ALIYEUAWA YAWAVAA POLISI

na Igenga Mtatiro, Tarime
FAMILIA ya diwani mstaafu wa Kata ya Kibasuka, Godfrey Gisururi (50), aliyeuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, imelishutumu Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa kushindwa kuwakamata watu hao.
Akizungumza na Tanzania Daima jana baada ya kumaliza mazishi, mtoto wa marehemu, Daniel Chagere, alisema tukio la kuuawa baba yake juzi kwa kupigwa risasi kichwani na kisha kukatwakatwa na mapanga ni la pili bila wahusika hao kuchukuliwa hatua na jeshi hilo.
Alisema tukio la kwanza lililotokea Aprili 22 mwaka huu, ambapo aliuawa kaka yake, Chacha Chegere na kwamba baada ya watu hao kufanya mauaji hayo walitoweka bila kumchukulia kitu chochote.
“Tukio la kwanza tuliwaambia polisi kwa majina waliohusika na mauaji hayo, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na sasa baba yetu ameuawa,” alisema Daniel.
Alisema watu hao wanaendeleza mauaji kwa kuwa wamewafichua, hivyo sasa wamejengewa chuki.
“Kinachotumaliza ni kuwafichua watu wanaoendesha uhalifu katika Jeshi la Polisi waliopo kijijini kwetu, sasa tumejutia kufanya hivyo, kwani tunashindwa kuelewa iweje siri hiyo ifichuke na kuambulia mauaji kila leo. Tunaomba watu hao wakamatwe la sivyo tunaomba ulinzi, kwani tunaishi kwa hofu,” alisema.
Naye kaka wa marehemu, Mwita Chegere, alimuomba mkuu wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, John Henjewele, kuwatumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwasaka watuhumiwa hao na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa