Home » » TEMBO WAVAMIA MAKAZI YA WATU SERENGETI, WAHARIBU MAZAO NA CHAKULA KILICHOHIFADHIWA

TEMBO WAVAMIA MAKAZI YA WATU SERENGETI, WAHARIBU MAZAO NA CHAKULA KILICHOHIFADHIWA

Mwandishi wetu, Mugumu-Mara Yetu
 
MAKUNDI makubwa ya wanayama aina ya Tembo kutoka katika pori la akiba ya Ikorongo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wamevamia katika makazi ya watu na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao, pamoja na chakula kilichohifadhiwa katika vijiji viwili vya kata ya Kabasa wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Diwani wa kata ya Natta Jumanne Kwiro Kinte, amesema jana kuwa wanyama hao wameingia kwenye makazi ya watu kwenye vijiji vya Montikeri na Makundusi na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao mashambani, ikiwa ni pamoja na kushambulia chakula cha wananchi ambacho kilikuwa kimehifadhiwa.
 
Kinte amesema kuwa kufuatia wanayama hao kuvamia makazi ya watu wananchi wa maeneo hayo sasa wanaishi kwa wasiwasi wakihofia kushambuliwa na kwamba kati ya wanyama hao yumo Tembo mmoja mkubwa ambaye ni dume ambaye amekuwa akitembea peke yake.

Amesema mbali na wanyama hao kuvamia mashamba ya wananchi katika vijiji hivyo na kushambulia mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula, pia wamevamia katika shule ya msingi Nyakitonyo na kushambulia mazao ya walimu yaliyokuwa mashambani.

Aidha amesema kuwa sasa hivi wakazi wa vijiji hivyo wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula na ameiomba Hifadhi ya Serengeti, pori la akiba la Ikorongo, pamoja na kampuni ya Grumeti Fund, kuwasaidia chakula wananchi ambao mazao yao yameshambuliwa na wanayama hao.

Meneja wa pori la akiba ya Ikorongo, Mathias Rwegasira, amekiri wanyama hao kuvamia maeneo hayo, ambapo pia amewaomba wananchi na viongozi wa maeneo ambako Tembo wanavamia, wawe wanatoa taarifa mapema ili hatua za kuwarudisha Hifadhini ziweze kuchukuliwa.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa