na Berensi Alikadi, Bunda
UKOSEFU wa
mitaji kwa wakulima, usimamizi imara wa watalamu na utashi wa kisiasa vimekuwa
vikichangia kushuka kwa uzalishaji wa zao la pamba wilayani Bunda kila mwaka.
Hayo
yalibainishwa mwishoni mwa wiki na washiriki wa mkutano wa kuboresha kilimo cha
pamba katika wilaya hiyo chini ya uenyekiti wa Mkuu wa wilaya hiyo, Joshua
Mirumbe.
Wakichangia
mada katika mkutano huo, baadhi ya wadau na wakulima wa zao hilo walidai wakulima
wengi hawana mitaji ya kuendeleza zao hilo na kwamba wengi wao wakishauza pamba
hutumia pesa zote na hata kukosa ya kununua pembejeo kwa msimu ujao.
Mkaguzi wa Bodi
ya Pamba wilaya za Bunda na Serengeti, Igoro Maronga, alisema suala la kilimo
cha pamba sasa hivi kimekosa usimamizi kuanzia kwa maofisa ugani hadi kwa
wanasiasa ambao pia wamekuwa hawalitilii maanani sana licha ya kufahamu kuwa
ndilo zao pekee linalowapa tija wapiga kura wao.
Igoro
alibainisha ukiukwaji wa masharti ya kanuni kumi za kilimo cha zao hilo, mbegu
kutochanganywa vizuri viwandani na kutoweka mbolea za samadi mashambani
kimekuwa chanzo kikubwa cha wakulima kupata mazao hafifu.
Naye Ofisa
Kilimo wa Kata ya Hunyari, Daudi Iramba, alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi
ya makampuni kuunda vikundi vya wakulima vijijini bila kuwahusisha wataalamu,
jambo ambalo limekuwa likiwapa shida maofisa ugani walioko vijijini katika
kufanya kazi na vikundi hivyo.
Akifungua
mkutano huo, Mkuu wa wilaya hiyo, Mirumbe, alisema lengo la mkutano huo ni kuweka
mkakati wa pamoja wa kuboresha zao la pamba ambalo ndilo zao la biashara kwa
wilaya hiyo ambapo hivi sasa uzalishaji wake unashuka kila mwaka.
Chanzo: Taaanzania Daima
0 comments:
Post a Comment