ASHINDWA KUTETEA KITI MARA, AMPA ANGALIZO MSHINDI, TARIMBA ATAMBA DAR, WAMBURA ATUPWA MAKONGORO Nyerere ameadhimisha vibaya kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha baba yake, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi wa kuwania Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara uliofanyika juzi na kumalizika usiku wa kuamkia jana. Jana ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 13 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga yaliyokwenda sanjari na kuzimwa kwa Mwenge wa Uhuru.
Katika uchaguzi huo wa Mkoa wa Mara, Makongoro aliyekuwa akitetea kiti hicho, alipata kura 422 na kuzidiwa na mpinzani wake wa karibu, Christopher Sanya aliyepata kura 481 huku tisa zikiharibika. Uchaguzi huo ilibidi urudiwe kwa kuwashindanisha wagombea wawili, kwani katika awamu ya kwanza wagombea wote hawakupata nusu ya kura kama kanuni za chama hicho zinavyotamka.
Awali, katika nafasi hiyo wagombea walikuwa watatu. Katika awamu ya kwanza, Sanya alipata kura 469, Makongoro (402) na mgombea mwingine, Enock Chambiri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara alipata kura 144. Baada ya matokeo hayo ya awali, Chambiri aliondoka ukumbini hapo. Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa, yalitangazwa na Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Nazir Karamagi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Makongoro alisema kuwa anakubaliana na matokeo hayo na kumuasa mshindi kufanya kazi kwa mujibu wa katiba. Pia alimtaka mshindi huyo kuvunja makundi aliyosema yameshamiri ndani ya chama hicho.
“Naomba uwe mwadilifu, Mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi. Kazi ya uenyekiti siyo lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo itatusaidia katika uchaguzi wa 2015.” “Wewe ndiye kiongozi mkuu wa mkoa huu wa kupanga uongozi katika uchaguzi mkuu hivyo ukishindwa tutayumba, tunaomba utoe ushirikiano na ukemee hii dhambi ya kukata majina, kwani inaweza ikaingia kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.”
Waliochaguliwa katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri ya Mkoa kupitia wilaya ni Josephat Seronga, Ester Nyarobi, Zuhura Makongoro, Jackson Waryoba, Josephat Kisusi na Felister Nyambaya. Wengine ni Grace Bunyinyiga, Thabita Idd, Abdallah Jumapili, Kananda Kananda, Mariam Mkono na Samson Gesase. Katika nafasi ya uenezi, Maximillian Ngesi amefanikiwa kutetea nafasi yake kama ilivyokuwa kwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Marwa Mathayo.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment