na Sitta Tumma
KATIKA
kukuza na kuboresha sekta ya michezo hapa nchini, Mbunge wa Musoma Mjini,
mkoani Mara, Vincent Nyerere (CHADEMA), amegawa vifaa mbalimbali kwa kata 13 za
jimbo hilo ikiwa ni maandalizi ya kuanzisha ligi itakayojulikana kama Nyerere
Cup.
Lengo
la michuano hiyo ni kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya kimichezo, kuibua
na kukuza vipaji vya vijana wa Musoma, ili baadaye waweze kuwa wachezaji wazuri
ndani na nje ya nchi.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya
Nyakato, Shule ya Msingi mjini hapa, Nyerere alisema tayari vifaa hivyo
vikiwamo jezi na mipira alishavitoa kwa kuwakabidhi maofisa watendaji wa kata
zote 13 za jimbo la Musoma mjini na kwamba viongozi hao wanatakiwa waandae
utaratibu mzuri wa kuwashirikisha vijana katika uundaji wa timu.
“Suala
la michezo kwa vijana wetu ni jambo zuri sana. Kwa hiyo nimeshaleta na
kuwakabidhi maofisa watendaji jimbo lote mipira na jezi kwa ajili ya kuanzisha
ligi ya jimbo.
“Nasikia
baadhi ya watendaji wameficha na hawataki kuwaelezeni kuhusu vifaa hivyo vya
michezo nilivyokabidhi. Sasa kupitia mkutano huu natoa onyo kwa mtendaji yeyote
ambaye amefungia vifaa hivi, ahakikishe anavigawa kwa vijana. Sijaleta kwa
ajili yao, nimeleta kwa ajili ya vijana wetu tuanzishe ligi ya jimbo,” alisema
mbunge huyo.
Alisema
kamwe hatashindwa wala kumuonea aibu ofisa mtendaji yeyote wa kata
atakayehujumu vifaa hivyo vya michezo alivyovitoa na kuwahakikishia wananchi wa
jimbo hilo, wakiwemo wapenda soka kwamba ataendelea kuwekeza pia kwenye michezo
ili kuinua sekta hiyo muhimu.
“Musoma
mjini kamwe sitakomea kuanzisha michuano ya soka jimboni hapa, bali
nitahakikisha na michezo mingine naifadhili ili kutoa fursa kwa vijana wengine
wanaopenda michezo mbalimbali kushiriki na hatimaye kuwa wachezaji wazuri wa
kitaifa na kimataifa, kisha kuliletea sifa jimbo, mkoa na taifa kwa ujumla,”
alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment