na Mwandishi wetu, Tarime
SERIKALI
imeupongeza mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya African
Barrick Gold (ABG) kwa juhudi zake za kutunza mazingira.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, alitoa
pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipofanya ziara kwenye mgodi huo ulioko wilaya
ya Tarime, Mara.
Katika
ziara hiyo Kitwanga aliongozana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen
Masele, ambapo uongozi wa mgodi ulieleza hatua mbalimbali unazochukua
kuhakikisha kunakua na mazingira salama.
“Hali
ya uhifadhi wa mazingira ni nzuri…wanapofanya uchimbaji wanahakikisha lile
vumbi halitoki popote wanapochimba na kumwaga maji kupunguza nguvu ya vumbi.
“Kwa
kweli wanajitahidi lakini kuna mambo kidogo inabidi tukubaliane ili kuhakikisha
wanakidhi viwango vya dunia hasa ISO 14001,” alisema Kitwanga alipozungumza na
waandishi wa habari.
Hata
hivyo imegundulika kuwa baadhi ya maeneo ya Tarime yameathirika na uchafuzi wa
mazingira unaotokana na matumizi ya kemikali ya zebaki inayotumiwa na
wachimbaji wadogo.
Uongozi
wa mgodi ulimweleza waziri huyo kuwa hautumii zebaki kwenye uzalishaji wake
badala yake hutumia kemikali ya cyanide.
“Kwa
kweli hili la wachimbaji wadogo nakubali kuwa wanahusika kwa sehemu katika
uharibifu wa mazingira. Cha kwanza ni kuwajengea mazingira ambayo yatawafanya
watumie hiyo zebaki lakini isitiririke katika vyanzo vya maji au mito yetu.
“Hilo
tumelizungumza na maofisa madini wa kanda na mikoa hii ili tuhakikishe
wanatumia mfuko wa wachimbaji wadogo ili wafanye shughuli zao kwa usalama,”
alisema naibu waziri huyo.
Kitwanga
alifanya ziara katika mgodi wa North Mara baada ya kuahidi kufanya hivyo kwenye
kikao cha Bunge kilichopita.
Katika
ziara hiyo, mawaziri hao walitembelea visima, shule na hospitali ya Sungusungu
iliyofanyiwa ukarabati na mgodi huo kwa gharama ya zaidi ya sh milioni 500.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment