na Sitta Tumma, Musoma
MBUNGE
wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), amewaondoa hofu wananchi wa jimbo
hilo, kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa na Chuo Kikuu cha Wauguzi
iliyopo jimboni humo na kusema miradi hiyo ipo mbioni kuanza kutekelezwa.
Nyerere
alisema hayo juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye
viwanja vya Nyakato Shuleni mjini Musoma na kuongeza kuwa taratibu zote za
kuanza ujenzi wa miradi hiyo imeshakamilika, kwani tayari wataalamu wa
kusimamia ujenzi huo wameshafika mjini Musoma.
“Ujenzi
wa hospitali yetu ya Rufaa ya Kwangwa na kile chuo cha Uuguzi ipo mbioni kuanza
kujengwa. Taratibu zote za ujenzi zimeshakamilika na juzi juzi hapa wataalamu
walifika kwa ajili ya upimaji tayari kwa utekelezaji wa kujengwa miradi hii ya
maendeleo.“Lakini, natumia mkutano huu kuwaonya wana CCM wanaowapotosha
wananchi kwamba eneo la hospitali na chuo hicho wamepewa wawekezaji. Huo ni
uzushi na uongo mtupu. Siasa na uongo zisiwepo kwenye maendeleo, ni bora
tutaniane sehemu nyingine, lakini isiwe kwenye maendeleo,” alisema.
Kwa
upande mwingine, Nyerere aliwahakikishia wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha
Mutex kulipwa fidia zao, kwani alishazungumza na Waziri wa Viwanda na Biashara,
Dk. Abdallah Kigoda, kuhusu kulipwa wafanyakazi hao na kwamba waziri huyo
alihidi bungeni kwamba serikali itawaongezea fedha za fidia tofauti na
ilivyowalipa awali.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment