Home » » Wanachuo 435 mwaka wa pili wagoma kula, Wanadai pesa walizonunulia vifaa vya kufundishia masomo kwa vitendo

Wanachuo 435 mwaka wa pili wagoma kula, Wanadai pesa walizonunulia vifaa vya kufundishia masomo kwa vitendo


WANACHUO cha ualimu Bunda, kilichoko mkoani Mara, Alhamisi wiki hii waligoma kula chakula cha jioni kutokana na madai mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa ratiba ya chakula kwa kutokupikiwa wali kama ratiba ilivyokuwa inaonyesha na badala yake wakapikiwa ugali.
Kufuatia hali hiyo jana Ijumaa polisi wakiwa wamejiandaa kwa mabomu ya machozi na silaha mbalimbali walifika chuoni hapo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Aidha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bunda, chini ya uenyekiti wa mkuu wa wiliya Joshua Mirumbe aliyewakilishwa na katibu tawala wa wilaya hiyo, Bw. Dominicus Lusasi ilifika chuoni hapo na kukutana na wanachuo hao ambao ni 435 wa mwaka wa pili.
Katika kikao hicho iliamriwa kuwa kuanzia sasa ratiba ya chakula ifuatwe na wanachuo hao siku zinazoonyesha ratiba ya kula wali wapikiwe chakula hicho.
 Wakizungumza katika kikao hicho, wanachuo hao wameyataja madai mengine kuwa ni kuhusu pesa zao walizotumia kunua vifaa vya kufundishia wakati wa mafunzo kwa vitendo kutokurudishiwa.

Wamesema kuwa wakati wa mafunzo kwa vitendo serikali ilikuwa haijaleta fedha za kununua vifaa vya kufundishia hali iliyowalazimu kila mwanachuo kutoa fedha zake na kununu vifaa hivyo, ili zoezi hilo liweze kwenda vizuri.

Wamesema kuwa sasa wanautaka uongozi wa chuo hicho uwalipe fedha hizo kwani tayari wizara ilikwishazituma na kwamba kila mwanachuo anatakiwa alipwe kiasi cha sh. 48,000.

Wameongeza kuwa madai mengine ni pamoja na michango mbalimbali wanayodaiwa kuchangishwa,licha ya kuwepo waraka wa serikali wakuzuia michango hiyo na kwamba sasa wanataka muafaka ili waweze kupewa fedha zao.

Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Bw. Josephat Rweyemamu,a amekanusha madai yote ya wanachuo hao na kusema kuwa fedha hizo za vifaa vya kufundishia wizara ilitoa agizo kuwa zinunue vifaa vya kufundishia na sio kuwapatia pesa tasilimu wanachuo hao.

Hata hivyo katibu tawala wa wilaya ya Bunda, alimwagiza mkuu wa chuo hicho kuiandikia barua wizara kuhusu madai ya wanachuo hao ya kuhusu fedha zao walizonunua vifaa vya kufundishia ili waweze kurejeshewa.

Baada ya kikao hicho wanachuo hao walikubali kukatisha mgomo wao huku wakiitaka serikali kushughulikia kero zao, hasa kero ya kulipwa fedha zao walizonunua vifaaa vya kufundishia.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa