MWANAUME mmoja amefikishwa
katika mahakama ya mkoa wa Mara, kwa tuhuma ya kukamatwa na CD zenye machapisho
ya kigaidi, ambazo zina mafunzo ya kijeshi na zinazochochea vurugu.
Aliyefikishwa katika mahakama
hiyo, ametambuliwa kwa jina la Ramadhan Twaha (36) mkazi wa mtaa wa Kirumba
jijini Mwanza.
Mwendesha mashitaka
wa serikali Bw. Jonas Kaijage, amemsomea mashitaka manne mshitakiwa huyo, mbele
ya hakimu mkazi, mfawidhi, mwandamizi wa mkoa wa Mara, Bw. Faisal Kahamba.
Bw. Kaijage amesema kuwa
mshitakiwa huyo anatuhumiwa kutenda makosa hayo septemba 27 mwaka huu,
katika msikiti wa Ibadhi ulioko mjini Bunda.
Amesema kuwa mshitakiwa huyo
anashitakiwa kusambaza CD zenye machapisho ya uchochezi, kuuza na
kushawishi watu kununua CD zenye picha na maelezo yasioruhusiwa kisheria,
pamoja na machapisho na picha zenye mwelekeo wa kigaidi na mafunzo ya kijeshi
kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa huyo amekana
mashitaka yote manne na kupelekwa mahabusu hadi tarehe 21 mwezi huu, kesi yake
itakapotajwa tena mahakamani hapo.
0 comments:
Post a Comment