Home » » Ugomvi wa wakulima na wafugaji wanukia

Ugomvi wa wakulima na wafugaji wanukia

WANANCHI katika Tarafa ya Kenkombyo wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wamesema kuwa kama wafugaji wanaolisha mazao yao hawatadhibitiwa iko siku utatokea mgogoro mkubwa, pamona na ugomvi kati ya wafugaji na wakulima.

 Wananchi hao wameyasema hayo juzi katika kijiji cha Kasahunga, kwenye kikao cha maendeleo kilichokuwa kimeandaliwa na mkuu wa wilaya ya Bunda, Bw. Joshua Mirumbe na kusimamiwa na Kaimu Afisa Tarafa ya Kenkombyo, Bw. Abiud Peter Jandwa.

Wamesema kuwa wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe kutoka katika maeneo mbalimbali, wamekuwa wakivamia mashamba yao na kulisha mazao, na kwamba kama hali hiyo itadhibitiwa mapema inaweza kusababisha mapigano kwa pande hizo mbili.

Wameongeza kuwa wafugaji hao kutokana na kukosa sehemu ya kulisha mifugo yao kwa sababu ya  ukame wamekuwa wakitoka maeneo mbalimbali na kuingiza kwa makusudi mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima nyakati za usiku ama  asubuhi, pindi wanapoona wenye mashamba hawako karibu.

Hata hivyo wananchi hao wamesema kuwa migogoro hiyo pia imekuwa ikisababishwa na baadhi ya viongozi wa ngazi ya kijiji na kata, baada yua kuruhusu makundi makubwa ya mifugo kuingia kwenye vijiji vyao, wakitokea vijiji vingine, baada ya kupewa chochote na wafugaji hao kwa maslahi yao binafsi.

Wakichangia hoja hiyo wananchi hao wamesema kuwa ni vema sheria na taratibu zikafutwa,  ikiwa ni pamoja na kila kijiji kutenga eneo lake la kuchungia mifugo, baadala ya maeneo mengi kutumika kwa kilimo, kama ilivyo kwa sasa.

Wameongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha wafugaji wa vijiji vingine kuvamia mashamba ya wakulima na kufanya uhalibifu mkunbwa wa mazao, ambapo hali hiyo ikiachwa iendelee, licha ya kutokea mapigano kati ya wafugaji na wakulima, pia itasababisha upungufu mkubwa wa chakula.

Akizungumzia kero hiyo, kaimu Afisa Tarafa ya Kenkombyo, Bw. Abiud Peter Jandwa, amesema kuwa amekuwa akipokea malalamiko hayo kutoka kwa wakulima, ambapo amewaonya viongozi wanaoruhusu makundi makubwa ya mifugo kuingia kwenye vijiji vyao na kusababishha kuwepo kwa migogoro hiyo.

Bw. Jandwa amewataka wafugaji wenye mifugo mingi kupunguza mifugo yao kwa kuiuza na kununua chakula, ili waweze kubaki na mifugo michache, ikilinganishwa na maeneo ya malisho yaliyopo kwwenye vijiji vyao.

Kikao hicho kilishirikisha viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi tarafa, vyama vya siasa na wadau mbalimbali wa maendeleo katika tarafa hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa