BAADHI ya walimu shule za sekondari katika wilaya ya
Bunda, mkoani Mara, wametuhumiwa kuwageuza wanafunzi wa kike kuwa wake
zao kwa kufanya nao mapenzi, hali ambayo imekuwa kero kubwa kwa wazazi na
walezi wa watoto hao.
Hayo yameelezwa juzi na kaimu afisa tarafa ya
Kenkombyo, Bw. Abiud Peter Jandwa, kwenye kikao kilichoshirikisha wadau
mbalimbali wa maendeleo wa tarafa hiyo, na kufanyika katika shule ya msingi
Kasahunga.
Bw. Jandwa aliyekuwa anamwakilisha mkuu wa wilaya ya
Bunda, Bw. Joshua Mirumbe, amesema kuwa amekuwa akipokea malalamiko mara kwa
mara, kutoka kwa wazazi na walezi juu ya kuwepo kwa hali hiyo.
Amesema kuwa wazazi na walezi hao wamekuwa wazkidai
kuwa kuna baadhi ya walimu wamegeuza watoto wa kike kuwa wake zao, hali ambayo
imekuwa ikisababisha wanafunzi hao kutokufanya vizuri katika masomo yao.
Kufuatia hali hiyo Bw. Jandwa amewaonya walimu wanaofanya
mchezo huo mchafu wa kufanya mapenzi na wanafunzi wao, kwani atakayebainika
ikiwa ni pamoja na kupatikana ushahidi wa kutosha atachukuliwa hatua kali za
kinidhamu na za kisheria.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kufuatilia mienendo
ya wanafunzi wao, ikiwa ni pamoja na kuwaonya kutokujiingiza kwenye vishawishi
ambavyo kwa namna moja ama nyingine wanaweza kukatisha masomo yao kwa kupata
ujauzito.
0 comments:
Post a Comment