WANANCHI katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara,
wameiomba serikali kutumia jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika
kukabiliana na uvuvi haramu hasa wa kutumia sumu katika ziwa Victoria, kwa
madai kuwa maafisa uvuvi pamoja polisi wameshindwa kuwadhibiti wavuvi hao.
Wananchi hao wameyasema hayo kwenye mkutano wa ndani
wa maendeleo uliokuwa umeandaliwa na mkuu wa wilaya ya Bunda, aliyewakilishwa
na kaimu Afisa Tarafa ya Kenkombyo, Bw. Abiud Peter Jandwa, na kufanyika katika
shule ya msingi Kasahunga.
Wamesema kuwa uvuvi haramu wa kutumia sumu, ambayo
sehemu kubwa ni dawa ya kuhifadhia maiti ya binadamu ili isiharibike,
umeshamiri sana katika Tarafa za Nansimio na Kenkombyo, hali ambayo
inahatarisha afya za binadamu pamoja na viumbe hai vingine vya majini.
Wameongeza kuwa kutokana na wavuvi hao kuwa na mbinuu
nyingi ikiwemo kuvua wakiwa wana silaha mbalimbali zikiwemo za jadi, sasa ni
vema jeshi la wananchi ilikaingilia kati na kuwasaka wavuvi hao, kwani
inaonekana maafisa uvuvi pamoja na polisi wameshindwa kukomesha hali hiyo.
Aidha, wamesema kuwa pamoja na kuwa mstari wa mbele
katika kukabiliana na wavuvi hao, lakini wanakatishwa tamaa na vyombo vya
serikali, wakiwatuhumu moja kwa moja polisi kwamba wamekuwa wakiwaachia huru
wavuvi hao hasa katika mazingira ya kutatanisha.
Wameongeza kuwa hivi karibuni wananchi wa kijiji cha
Buzimbwe pamoja na wanajeshi wa JKT, walipambana na wavuvi hao waliokuwa na
pinde na mawe na kufanikiwa kuwakamata watatu, huku wawili wakijitosa majini,
ambapo mmoja alikufa maji.
Wamesema kuwa cha ajabu wavuvi watatu waliokamatwa na
kupelekwa polisi inadaiwa wameachiwa huru, ingawa walikuwa na vielelezo vyao,
ikiwemo sumu pamoja na samaki ambao tayari walikuwa wameshavuliwa.
Wamefafanua kuwa hiyo ni mara ya pili kwa
wavuvi hao kukamatwa, ambapo kesi nyingine ya kwanza na yenyewe
walidhaminiwa katika mazingira ya mashaka.
Kamanda wa polisi mkoani mara, kamishina msaisdizi wa
polisi, Bw. Ferdinand Mtui, amesema kuwa atafuatilia suala hilo kwa ukaribu
zaidi, ili kupata ukweli wake.
0 comments:
Post a Comment