Home » » Familia kuwaburuza kortini askari TANAPA

Familia kuwaburuza kortini askari TANAPA



FAMILIA ya marehemu Peter Maseya imekusudia kuwaburuza mahakamani askari wa Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) katika Hifadhi ya Serengeti kwa madai ya kumuua ndugu yao kwa tuhuma za ujangili.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa usiku wa kuamkia Oktoba 16, mwaka huu na askari hao  baada ya kumvamia nyumbani kwake, kumteka na kumtesa hadi kumuua akiwa kijijini kwake Murito-Nyamongo, wilayani Tarime, Mara.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Chacha Masero, alisema wanachosubiri sasa ni kukamilisha ushauri wa kisheria pamoja na kupata majibu ya uchunguzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
“Familia inaendelea kukamilisha hatua za kisheria za kuwafikisha mahakamani askari waliofanya mauaji ya ndugu yetu… lakini pia tunasubiri majibu ya kichunguzi yanayofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kupitia viongozi wake wakubwa ambao tuliwaeleza tukio zima,” alisema Masero.
Akisimulia mkasa huo, Masero alisema Maseya alivamiwa akiwa nyumbani kwake saa nane usiku, Oktoba 13, mwaka huu na askari hao wapatao watano ambao walimchukua pamoja na watoto wake watatu na mfanyakazi wake.
“Askari hao walimtesa baba yetu, mmoja wao alitufuata na kutueleza kuwa baba hataki kusema na kutuambia twende tukapewe urithi wetu kabisa,” alisema.

CHANZO;TANZANIA DAIMA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa