WANANCHI
katika Wilaya Tarime mkoani Mara, wameiomba serikali kukomesha wizi wa
mifugo unaotokea mara kwa mara wilayani humo, ambao unadaiwa kufanywa na
watu kutoka nchi jirani.
Wakizungumza na waandishi wa habari wananchi hao waliokuwa
wanafuatilia ng’ombe 10, walioibwa juzi, walidai kuwa wezi hao wanatoka
nchi jirani ya Kenya ambapo waliibwa katika Kijiji cha Murito, kilichoko
wilayani humo.
Walisema kuwa tabia ya wizi wa mifugo imekuwa ikijitokeza mara kwa
mara huku wezi hao wakiwapeleka nchini humo, hivyo waliiomba serikali
kuhakikisha wanaweka ulinzi madhubuti ili kukomesha matukio hayo kwani
katika kipindi cha miaka miwili zaidi ya ng’ombe 800 wameibwa.
“Wezi hao baadhi yao wanatoka nchi jirani, tena wengine wana makazi
ya sehemu mbili; hapa nchini na Kenya, tunaomba serikali itusaidie
kukomesha hali hii,” alisema.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Tarime na Rorya, Justus Kamugisha, alisema kuwa juhudi
zinafanyika kukomesha tabia hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya mawasiliano
na askari wa Kenya ili kuhakikisha wezi hao wanakamatwa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment