Home » » NEIT YAANDIKISHA WAKULIMA WANAOTAKA KUKOPA MBOLEA

NEIT YAANDIKISHA WAKULIMA WANAOTAKA KUKOPA MBOLEA

Taasisi ya mfuko wa uwekezaji kiuchumi katika tarafa ya Nyanja (NEIT) wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara imeanza zoezi la kuorodhesha wakulima katika wilaya hiyo ili kuwapatia kwa mkopo mbolea ya minjingu mazao itakayowasaidia katika kilimo cha mazao mbalimbali.

Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya NEIT bw. Steven Machumu amesema kwamba zoezi hilo limeanza tangu mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo wakulima wa mazao mbalimbali ambao ni wanachama wa mfuko huo wanatakiwa kujiorodhesha mapema kupitia vikundi vyao vilivyo katika kila kata wilayani humo.

Bw. Machumu amesema kuwa mfuko wa NEIT umekubaliwa  na menejimenti ya kiwanda cha mbolea aina ya minjingu kilichopo mkoani Manyara kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo ya mbolea kwa wakulima kwa masharti nafuu lengo likiwa ni kutokomeza umasikini na upungufu wa chakula katika wilaya hiyo ya Musoma Vijijini.

Mfuko huo wa uwekezaji kiuchumi unatarajia kuwekeza zaidi ya sh bilioni 52 katika sekta mbalimbali kwenye kata 17 za wilaya hiyo ikiwa ni mkakati wa kupunguza umaskini unaowakabili wananchi ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara yakiwemo kama vile mahindi,mpunga,viazi vitamu,pamba na mboga mboga.

Bw. Machumu amesema kwamba utekelezaji wa mkakati huo unatarajiwa kuzinduliwa rsmi mwezi January mwakani ambapo hadi hivi sasa vikundi 63 vya ujasiliamali na maendeleo vimekwisajiliwa katika taaasisi kama wanachama na kufungua akaunti zao benki.

Amefafanua kuwa NEIT itasaidia kupunguza umasikini wa wananchi wa kata 17 za wilaya ya Musoma Vijijini katika sekta za Kilimo,Uvuvi,Ufugaji,Mazingira,Elimu na Afya ambapo miradi mikubwa kupitia sekta hizo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ya mradi unaoanza mwaka huu wa fedha wa 2013/14.

Amesema lengo la uwekezaji huo ni kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi walio wengi vijijini wanaoabiliwa na umaskini mkubwa ambapo baadhi ya miradi mikubwa iliyolengwa kutekelezwa katika mkakati huo ni mapinduzi ya kijani katika sekta ya kilimo kwa kushirikiana na serikali katika mpango wake wa KILIMO KWANZA kupitia ASDP na DADIPS.

Ameitaja miradi mingine itakayotekelezwa kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa benki kata(SACCOS), benki ya Exim ambayo tayari imeshaonesha nia ya kujenga tawi katika wilaya hiyo,boti za uvuvi za kisasa,ujenzi wa chuo cha mafunzo ya kilimo,chuo cha uuguzi na afya sanjari na ujenzi wa vituo 3 vya afya.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa