MAENDELEO duni, uchu wa madaraka, mila potofu na usimamizi mbovu wa
sheria kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi za taifa, imetajwa
kuwa ni kichocheo kikubwa cha migogoro kati ya Shirika la Umma la
Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), na jamii husika.
Hayo yalibainishwa jana na mwezeshaji wa semina ya mafunzo kwa
waandishi wa habari inayoendelea mjini hapa, ambaye pia ni Mkurugenzi
wa Tanzania Audio-Visual and Communication Menejimenti, Charles Kayoka,
wakati alipozungumzia chanzo cha migogoro.
Kayoka alisema hali hiyo inatakiwa kukomeshwa kwa kila mamlaka husika
kuwajibika ipasavyo katika suala zima la kusogeza huduma karibu za
kimaendeleo kwa jamii yote, ikiwemo inayozunguka hifadhi za taifa.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mbali na hayo viongozi wa halmashauri
zinazozunguka maeneo hayo ya hifadhi za taifa, hawana budi kuwajibika
katika kuboresha huduma kwa wananchi wao.
“Migogoro mingi katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi za taifa,
inasababishwa na mfumo duni wa maendeleo, usimamizi mbovu wa sheria,
wanasiasa na mambo mengine kama vile mila potofu.
“Kwa hali hii, halmashauri lazima ziwajibike kuhakikisha zinaboresha
mfumo bora wa kiuchumi kwa wananchi wao. Suala hili siyo la TANAPA
pekee,” alisema Kayoka.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichangia asilimia
17.5 katika fedha zote zinazopatikana katika pato la taifa, hivyo ni
lazima maeneo ya hifadhi yaheshimiwe kwa mujibu wa sheria za nchi.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, waliwalaumu waandishi wa habari
kwa kufanya kazi zao maeneo ya mijini na kushindwa kufika katika maeneo
ya vijijini ambako kuna mahitaji na migogoro mingi.
Mhariri wa habari wa gazeti la Rai, Masyaga Matinyi pamoja na Naibu
Mhariri Mtendaji gazeti la Jamhuri, Jackton Manyerere, walisema kamwe
tatizo la ujangili halitaisha iwapo serikali haitawajibika kuchukua
hatua za kisheria kwa wanaoonekana kuhusika na hujuma hizo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment